Mshauri mwandamizi wa Umoja wa Mataifa alisema Ijumaa kuwa kila dakika, hekta 23 za ardhi zinaharibiwa na ukame na kuongezeka kwa jangwa. Alisema hali hiyo inaathiri misingi ya uchumi, kijamii na mazingira yanayohitajika kwa maendeleo.
Luc Gnacadja, katibu mtendaji wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayopambana na kuongezeka kwa jangwa alikuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano uliofanyika Algeria. Akizungumza katika mkutano huo alisema maeneo ya majangwa ya asili ni muhimu pia kwa mazingira lakini kuongezeka kwa jangwa kunakosababishwa na watu ndio kunaleta athari zaidi.
"Hali hiyo inaathiri vibaya uwezo wetu katika kupambana na umasikini, na uwezo wetu wa kupambana kuongezeka kwa ukame," alisema.
Kuharibika kwa ardhi, alisema bwana Gnacadja, kunatishia uwezo wa ardhi kuhifadhi maji - na hivyo hata maisha ya viumbe vingine duniani licha ya binadamu. Kunasababisha pia watu kuhama hama kutokana na madhara ya mazingira na hivyo kutishia usalama wa chakula kwa binadamu.