Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 15:41

Guterres kuhutubia baraza la Usalama la UN Jumatano


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres Jumatano atatoa taarifa kwa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu hatua ya hivi karibuni ya Ethiopia ya kuwafukuza maafisa saba waandamizi wa mashirika ya misaada ya Umoja wa mataifa.

Utakuwa mkutano wa pili wa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu Ethiopia chini ya wiki moja, ambapo serikali kuu ya waziri mkuu Abiy Ahmed ilitangaza hapo tarehe 30 Septemba kwamba maafisa hao wa misaada wamepewa saa 72 kuondoka nchini humo.

“Kufukuzwa kwa wafanyakazi hawa wa misaada ni hatua moja nyingine ya kasi ambayo inachukuwa mwelekeo mbaya juu ya hali kuzidi kuzorota,” amesema balozi wa Ireland kwenye Umoja wa mataifa Geraldine Byrne Nason, aliyeomba mkutano huo kwa niaba ya serikali yake.

Byrne Nason amesema ni muhimu maafisa hao wa misaada warejeshwe kwenye nafasi zao na uhusiano kati ya Umoja wa mataifa na serikali ya Ethiopia uboreshwe.

Ethiopia ilidai maafisa hao waliingilia masuala yake ya ndani na kuongeza tuhuma nyingine, ikiwemo kwamba walitoa misaada na vifaa vya mawasiliano kwa waasi wa Tigray People’s Liberation Front ( TPLF), ambao serikali imekuwa ikipigana nao kaskazini mwa nchi kwa karibu mwaka mmoja.

Maafisa waliofukuzwa ni pamoja na naibu mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na misaada ya kibinadamu, naibu mratibu wa misaada ya kibinadamu, na mwakilishi wa shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia watoto ( UNICEF).

Jumatatu, Umoja wa mataifa ulithibitisha kwamba maafisa hao hawapo tena nchini Ethiopia.

XS
SM
MD
LG