Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Oktoba 10, 2024 Local time: 19:54

Guterres aomba Ethiopia iruhusu upelekaji misaada bila pingamizi


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres Jumatano ameitaka serikali ya Ethiopia kuruhusu utoaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu kaskazini mwa nchi bila pingamizi.

Hayo yanajiri wakati maafisa wa Umoja wa mataifa wakiripoti vifo kutokana na njaa.

Wakati wa mkutano wa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa, Guterres amesihi serikali ya Ethiopia kuruhusu usambazaji usiokuwa na kizuizi wa mafuta yanayohitajika, pesa taslimu, vifaa vya mawasiliano pamoja na misaada ya kibinadamu huko Tigray, Amhara na Afar.

“Wenzetu ambao wako uwanjani wanatufikishia ushahidi wa kutisha wa watu kuhusu mateso, ikiwemo maelezo ya vifo vinavyohusishwa na njaa”, Guterres amesema.

Wajumbe 15 wa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa wamekutana jana baada ya serikali ya Ethiopia kuwafurusha wiki iliyopita, maafisa waandamizi saba wa Umoja wa mataifa kwa madai ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Umoja wa mataifa ulipinga hatua hiyo na kusema hakuna ushahidi wa kuunga mkono madai hayo ya serikali ya Ethiopia.

Vita vilizuka miezi 11 iliyopita kati wanajeshi wa serikali kuu ya Ethiopia na wanajeshi watiifu kwa chama cha TPLF, ambacho kinadhibiti jimbo la Tigray. Maelfu ya watu wamefariki huku, mamillioni ya wengine wakitoroka makazi yao wakati mzozo ukienea kwenye majimbo jirani ya Amhara na Afar.

Guterres amesema watu millioni 7 wa Tigray, Amhara na Afar wanahitaji msaada, wakiwemo watu millioni 5 huko Tigray ambako watu laki 4 wanakadiriwa kuishi katika mazingira ya njaa.

XS
SM
MD
LG