Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 18, 2024 Local time: 03:32

Rais Conde asema analiamini jeshi lake


Makazi yaliyoharibiwa ya Rais wa Guinea, Alpha Conde, katika mji wa Conakry wakati wa jaribio la kutaka kumuuwa lililofanywa na waasi Julai 19,2011
Makazi yaliyoharibiwa ya Rais wa Guinea, Alpha Conde, katika mji wa Conakry wakati wa jaribio la kutaka kumuuwa lililofanywa na waasi Julai 19,2011

Rais wa Guinea Alpha Conde anasema analiamini jeshi lake licha ya jaribio lililoshindikana la kutaka kumuua lililofanywa na wanajeshi waasi wiki mbili zilizopita.
Katika mahojiano na Idhaa ya Kifaransa ya Sauti ya Amerika bwana Conde alisema jeshi linafanyiwa mabadiliko na hivi sasa ni jeshi la kitaifa ambalo liko chini ya udhibiti wa kiraia.

Rais alisema baadhi ya maafisa wa cheo cha juu hawayapendi mabadiliko haya na katika maneno yake “walifikiria kifo changu kitairudisha Guinea katika kipindi kibaya kilichopita”.

Lakini bwana Conde aliongeza kuwa huwezi kusitisha historia kujirudia.
Bwana Conde aliepuka mashambulizi mawili nyumbani kwake katika mji mkuu Conakry hapo Julai 19.

Maafisa wa usalama nchini Guinea walisema wiki iliyopita kuwa wamewakamata watu 38 kuhusiana na mashambulizi hayo, watu 25 ni wafanyakazi wa jeshi. Mtu wa kwanza kukamatwa alikuwa mkuu wa zamani wa jeshi Jenerali Nouhou Thiam.

Bwana Conde alichaguliwa kuwa Rais Novemba mwaka jana katika uchaguzi wa kwanza huru na wa haki nchini Guinea tangu ipate uhuru mwaka 1958.

Nchi ya Guinea awali ilikuwa na historia ya utawala wa kibabe na mapinduzi ya mara kwa mara. Mapinduzi ya hivi karibuni yalitokea Disemba mwaka 2008 wakati kundi moja la maafisa wa jeshi walipochukua madaraka baada ya kifo cha kiongozi wa muda mrefu Lansana Conte.

Bwana Conde alizungumza na Sauti ya Amerika-VOA, Jumapili siku mbili baada ya yeye na marais watatu wengine wa nchi za Afrika magharibi kukutana na Rais Obama huko Ikulu nchini Marekani.

Alisema alimwambia bwana Obama kwamba nchi ya Guinea itafanya kila kitu kuingia katika uwanachama wa mkataba wa kibiashra wa nchi Afrika unaowezesha nchi za Afrika kufanya biashara na Marekani , pamoja na na ule wa Millenia unaofadhiliwa na Marekani kusaidia nchini zinazoendelea barani Afrika.

Pia alisema ataendelea kuiweka Guinea katika njia ya demokrasia. Bwana Conde anatarajiwa kuondoka Washington Jumatatu.

XS
SM
MD
LG