Upatikanaji viungo

Alhamisi, Februari 29, 2024 Local time: 22:44

Upinzani Guinea Bissau wakataa spika kuwa Rais wa muda


Spika wa bunge nchini Guinea Bissau, Raimundo Pereira
Spika wa bunge nchini Guinea Bissau, Raimundo Pereira

Vyama vya upinzani nchini Guinea Bissau vinapinga spika wa bunge nchini humo kuwa Rais wa muda kwa mujibu wa katiba ya nchi

Siku moja baada ya kifo cha Rais wa Guinea Bissau, Malam Bacai Sanha, vyama vya upinzani vinakataa mpango wa spika wa bunge kuhudumu kama rais wa muda.

Chini ya katiba, mkuu wa bunge anatakiwa kuhudumu kama kiongozi wa muda na kupanga uchaguzi ambao unatakiwa kufanyika ndani ya muda wa siku 90 kufuatia kifo cha rais. Lakini Jumanne, kundi moja la vyama vya upinzani limetoa taarifa ikikataa kiongozi wa bunge, Raimundo Pereira, kama rais wa muda.Vyama vinahoji kama Peraira atakuwa mwaminifu kufuata katiba.

Kifo cha bwana Sanha kimezusha wasi wasi wa kung’ang’ania madaraka katika taifa hilo dogo la Afrika magharibi linalojulikana kwa historia yake ya hali tete ya kisiasa na ghasia. Mkuu wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi-ECOWAS, ametoa wito wa kuwepo hali ya utulivu na kufuata taratibu za katiba ya nchi za kukabidhiana madaraka.

Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, mkuu wa ECOWAS, James Gbagho alisema kundi litaendelea kuiangalia Guinea Bissau kwa karibu zaidi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita darzeni ya wafanyakazi wa jeshi walikamatwa baada ya kushukiwa kufanya jaribio la mapinduzi. Wote waliokamatwa akiwemo mkuu wa jeshi la majini nchini humo, Bubo Na Tchuto, ambaye alishutumiwa kwa kupanga njama hizo.

Marehemu bwana Sanha alichaguliwa kuchukua nafasi ya Rais Joao Vieira ambaye aliuwawa na wanajeshi waasi mwezi Machi mwaka 2009. Bwana Sanha alifariki Jumatatu katika hospitali moja mjini Paris nchini Ufaransa, ambapo alikuwa akipatiwa matibabu juu ya afya yake ambayo haikuelezwa bayana.

XS
SM
MD
LG