Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 29, 2023 Local time: 06:59

Ghasia zaongezeka Jamhuri ya Afrika ya Kati


Mama huyu alia baada ya dadake kuuawa katika ghasia mjini Bangui February 9, 2014.

Takriban wanajeshi 1,600 wa Ufaransa na 6,000 wa Umoja wa Afrika wamo nchini humo kujaribu kulinda raia wakati ghasia zenye maafa zikiendelea kati ya Wakristo na Waislam

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa anasema lazima tahadhari zichukuliwe ili Jamhuri ya Afrika ya Kati isigawanyike. Onyo hilo limetolewa huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakionya kuwa mauaji ya kikabila yanaendelea katika taifa hilo lililokumbwa na mgogoro wa kisiasa.

Waziri huyo Jean Yves Le Drian alifanya mazungumzo mjini Bangui na maafisa wa ngazi ya juu ya jeshi la Ufaransa pamoja na kaimu rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba- Panza aliyeungana naye wakati wa ziara yake kusini magharibi mwa nchi.

Hii ni mara ya tatu kwa waziri Le Drian katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, tangu Ufaransa ilipozindua operesheni ya kijeshi mwishoni mwa mwaka jana. Onyo lake limetolewa huku makundi mawili ya kutetea haki za binadamu Amnesty International na Human Rights Watch yakionya juu ya mauaji ya kikabila katika baadhi ya maeneo ya nchi yanayolenga waislam walio wachache.

Akizungumza na kituo cha televisheni ya Ufansa France 24, kamishina wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi Antonio Guterres alisema hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ni janga la kibinadamu. Alitoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuongeza idadi ya walinda amani haraka ili kurejesha uthabiti nchini humo.

Takriban wanajeshi 1,600 wa Ufaransa na 6,000 wa Umoja wa Afrika wamo nchini humo kujaribu kulinda raia wakati ghasia zenye maafa zikiendelea kati ya Wakristo na Waislam. Jumuiya ya Ulaya inategemewa kupeleka wanajeshi 500 katika mji mkuu Bangui mapema mwezi Machi.

Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alisema ameomba Ufaransa kupeleka wanajeshi zaidi nchini humo kuzuia ghasia hizo kuendelea. Takriban watu 1,000 wameuawa na maelfu kutoroshwa makazi yao.
XS
SM
MD
LG