Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 17:27

Gbagbo apiga marufuku ndege za UN nchini kwake


Alassane Ouattara, Rais aliyeidhinishwa na UN
Alassane Ouattara, Rais aliyeidhinishwa na UN

Rais Laurent Gbagbo anayeng’ang’ania madaraka nchini Ivory Coast, jana alhamisi amepiga marufuku ndege za Umoja wa Mataifa kuruka katika anga ya nchi hiyo, hatua ambayo inaweza kufanya iwe vigumu kwa Alassane Ouattara kurudi nyumbani akitokea Ethiopia.

Wakati huo huo Rais anayetambuliwa kimataifa nchini Ivory Coast, Alassane Ouattara, anasema jopo la ngazi ya juu la Umoja wa Afrika limethibitisha kwamba alishinda uchaguzi uliokuwa na utata nchini humo. Bwana Ouattara alisema kwamba jopo hilo pia lilimtaka kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa na kumpa fursa Rais Laurent Gbagbo kuondoka kwa heshima.

Umoja wa Mataifa ilimuidhinisha bwana Ouattara, kama mshindi wa uchaguzi wa Rais wa mwezi Novemba, lakini bwana Gbagbo anakataa kukabidhi madaraka. Jopo la AU linalojumuisha marais watano wa nchi za Afrika, halikutangaza hadharani uamuzi wake baada ya kukutana huko Ethiopia. Hata hivyo shirika la habari la Associated Press linaripoti kwamba maafisa kutoka pande zote za serikali zinazoshindana huko Ivory Coast wamethibitisha jopo lilimuunga mkono bwana Ouattara kama rais.

Bwana Ouattara alihudhuria mkutano huko Addis Ababa siku ya Alhamisi, lakini bwana Gbagbo hakushiriki. Wawakilishi wa Gbagbo walisema kabla hata ya mkutano kuanza kwamba alilikataa pendekezo la AU kumaliza mtafaruku.

XS
SM
MD
LG