Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 31, 2024 Local time: 01:16

Gbagbo awekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa


Wanajeshi wanaomuunga mkono Allasane Ouattara.
Wanajeshi wanaomuunga mkono Allasane Ouattara.

Wanachama wa baraza hilo la UsaIama walimwekea Gbagbo udhibiti wa mali na kutoa marufuku ya kusafiri

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kwa kauli moja Jumatano jioni, kuweka vikwazo dhidi ya rais anayeng’ang’ania madaraka wa Ivory Coast Laurent Gbagbo, na ambaye amepuuzilia mbali mwito wa jamii ya kimataifa wa kuyaachia madaraka kwa kiongozi anayetambulika kimataifa kama mshindi halali wa uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba mwaka jana.

Mwandishi wa VOA Margaret Besheer anaripoti kutoka makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuwa azimio nambari 1975 linatoa mwito kwa Bw.Gbagbo kuheshima maamuzi ya raia wa Ivory Coast na kuondoka madarakani na kumwachia mshindi wa kiti hicho Alassane Ouattara aliyethibitishwa na Umoja wa Mataifa kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Azimio hilo lililoidhinishwa Jumatano limewasihi walinda amani takriban elfu-10 walioko nchini Ivory Coast kutumia kila njia kulinda raia kutokana na vitisho na ghasia.

Na katika hatua ya kuhimiza shinikizo kwa Bw.Gbagbo wanachama 15 wa baraza hilo la UsaIama walimwekea Gbagbo udhibiti wa mali na kutoa marufuku ya kusafiri dhidi yake, mkewe na washirika wake watatu.

Ufaransa na Nigeria zilidhamini kwa pamoja azmio hilo. Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Gerard Araud aliwaambia waandishi habari kuwa hali nchini ivory Coast inazidi kuwa tete saa baada ya saa.

Umoja wa Mataifa unasema watu 462 wameuawa tangu mzozo wa kisiasa kuibuka tena mapema mwezi Desemba. Zaidi ya watu milioni moja wamefurushwa makwao, na maelfu sasa ni wakimbizi katika nchi za Ghana na Liberia.

XS
SM
MD
LG