Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 15, 2024 Local time: 08:48

Waasi Libya waiteka Tripoli


Waasi nchini Libya wameteka kituo kikuu cha kijeshi ambacho kinalinda ngome kuu ya Moammar Gadhafi mjini Tripoli. Jumapili Agosti 21, 2011
Waasi nchini Libya wameteka kituo kikuu cha kijeshi ambacho kinalinda ngome kuu ya Moammar Gadhafi mjini Tripoli. Jumapili Agosti 21, 2011

Wapiganaji wa upinzani nchini Libya wameuteka mji mkuu Tripoli na kuwashikilia watoto wawili wa Gadhafi

Wapiganaji wa upinzani nchini Libya wameingia kati kati ya mji mkuu wa Libya Tripoli na kunyakuwa uwanja mkuu wa kijani baada ya kuingia ndani ya mji huo Jumapili usiku bila ya kukabiliwa na upinzani wowote wa kijeshi.

Wapiganaji hao walitangaza kwamba watoto wawili wa kiume wa Moammar Gadhafi wamekamatwa akiwa ni pamoja na aliyetarajiwa kurithi nafasi yake Seif al-Islam.

Wapiganaji wa upinzani walipofika katika mipaka ya mji mkuu kutokea magharibi hawakukabiliana na upinzani mkubwa walipokuwa wanapita mbio kwenye vituo muhimu vilivyokuwa vinashikiliwa na vikosi vya serikali nje ya mji mkuu.

Maelfu ya wakazi wa Tripoli wamekuwa wakisherehekea usiku kucha wakati wapiganaji walipoingia katika uwanja mashuhuri ambao wameubadilisha jina lake mara moja na kuitwa uwanja wa mashujaa ambako wa Libya waliokuwa na furaha walianza kuangusha na kuharibu mabango makubwa ya picha ya bwana Gadhafi na kuanza kuyakanyaga.

Hadi hivi karibuni serikali ya Libya imekuwa ikiutumia uwanja huo kuanda maandamano makubwa ya wananchi kuonesha uungaji mkono wa kiongozi wa Libya ambaye anaonekana kuwa ameshindwa hivi sasa.

Viongozi wa upinzani hata hivyo wamekiri alfajiri ya Jumatatu kwamba kungali kuna maeneo ambayo kuna upinzani ndani na nje ya Tripoli. Msemaji wa upinzani amesema wapiganaji wameshauzingira uwanja wa Bab Alazizya ambako wanaamini huwenda bwana Gadhafi amejificha lakini wanasita kuanza kushambulia.

Msemaji wa waasi anasema walipeleka kundi la wapiganaji kuingia katika mji mkuu kupitia bahari kutokea bandari ya Misrata. Aliongeza kusema kwamba kikosi maalum cha ulinzi wa Gadhafi kimejisalimisha na hivyo kuwawezesha wapiganaji kuchukua udhibiti wa sehemu kubwa ya mji.Jumapili mahakama ya uhalifu wa kimataifa-ICC ilithibitisha kukamatwa kwa Seif al-islam. Anashtakiwa pamoja na baba yake na mkuu wa ujasusi wa Libya kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu kwa madia ya kupanga na kuamrisha mashambulio yasiyo halali dhidi ya raia siku za mwanzoni mwa upinzani wa wananchi ambapo serikali iliwakandamiza kikatili wapinzani wa serikali.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Luis Moreno Ocampo alisema Jumapili kwamba ni lazima kwa Seif Al-islam kukabidhiwa kwenye mahakama ya The Hague haraka iwezekanavyo. Wakati huo huo viongozi wa upinzani waliwambia waandishi wa habari kwamba kijana mkuu wa Gadhafi, Mohammed alijisalimisha mwenyewe kwa vikosi vya upinzani.

Jumapili televisheni ya taifa nchini Libya ilitangaza ujumbe kadhaa wa bwana Gadhafi akieleza ukaidi wake dhidi ya upinzani. Ujumbe wa mwisho alikiri kwamba vikosi vya upinzani vimesonga mbele na kuingia Tripoli na kuonya kwamba mji huo mkuu utageuka kuwa Baghdad nyingine. Kiongozi huyo wa Libya alisema atabaki ndani ya mji mkuu hadi mwisho kulinda mji na alitoa wito kwa wafuasi wake kusaidia kuukomboa.

Maelfu ya watu walikusanyika mapema Jumatatu katika mji wa Benghazi, mji mkuu wa upinzani huko mashariki ya Libya wakati ripoti zilipokuwa zinazidi kutolewa juu ya kufanyika uvamizi katika mji wa Tripoli na matumaini kwamba mwisho wa Ghadafi umefika.

XS
SM
MD
LG