Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Februari 23, 2024 Local time: 13:27

Fujo katika bunge la Kenya kila upande ukidai kuwa na wabunge wengi


Maafisa wa kukabiliana na ghasia wakishika doria nje ya majengo ya bunge la Kenya wakati wa mjadala kuhusu mswada wa usalama Dec 18 2014. Picha: AFP
Maafisa wa kukabiliana na ghasia wakishika doria nje ya majengo ya bunge la Kenya wakati wa mjadala kuhusu mswada wa usalama Dec 18 2014. Picha: AFP

Fujo zimeshuhudiwa katika Bunge la Kenya baada ya Spika Moses Wetang’ula kuamuru kuwa Muungano wa Rais William Ruto wa Kenya Kwanza ndio unaostahili kuchukua Kiongozi wa walio Wengi kutokana na makubaliano ya kisiasa na vyama tanzu vilivyogura Muungano wa Odinga baada ya ushindi wa Ruto.

Wabunge kadhaa wa Upinzani wa Muungano wa Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya wamemfokea vikali Spika aliyelazimika kuahirisha kikao cha bunge hilo kwa ghafla.

Spika wa bunge la Kitaifa la Kenya Moses Masika Wetang’ula amelazimika kukatiza ghafla kikao cha bunge cha Alhamisi hadi Jumanne wiki ijayo baada kuibuka kizazaa na makabiliano makali kutoka kwa wabunge wa upinzani wa Muungano wa Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya walioonekana kumzomea vikali Bw Wetang’ula kwa kutoa uamuzi usiowaridhisha, kuwa kwa misingi ya makubaliano ya kisiasa ya baada ya uchaguzi mkuu, yaliywafanya wabune 14 kugura Muungano wa Odinga, Muungano wa Rais William Ruto wa Kenya Kwanza ndio utakaochukua wadhifa wa Kiongozi wa Walio Wengi katika bunge hilo.

Kwa dakika kadhaa, hata baada ya spika Wetang’ula kuamuru kuwa maamuzi yake hayawezi kupingwa au kujadiliwa kwa hoja za nidhamu ndani ya bunge hilo, wabunge wa upinzani walionekana kuondokea viti vyao na kusimama pembeni mwa bunge hilo kuliko na Mesi ya bunge ambacho ni kielelezo cha mamlaka ya Spika na Bunge la Taifa, na hivyo basi kuwalazimu wapambe wa bunge hilo kukizingira na kumlazimu Wetang’ula kukatiza kikao hicho kwa ghafla hivyo basi kukatiza hoja iliokuwa inafuata ya kujadili hotuba ya rais.

Wabunge waliohama muungano wa Odinga na kujiunga na Ruto

Kabla ya kizazaa hicho, Wetang’ula ambaye ni mojawapo wa viongozi wa Muungano wa Kisiasa wa rais Ruto, katika maamuzi yake, ameeleza kuwa itakuwa si busara kuwa wabunge 14 waliochaguliwa kuingia bungeni chini ya vyama vilivyokatiza uhusiano wao na Muungano wa Odinga kisheria kutojumuishwa chini ya mkataba wa kisiasa na Muungano wa Ruto.

Spika Wetang’ula anaeleza kuwa vyama vya United Democratic Movement, Pamoja African Alliance (PAA), Maendeleo Chap Chap Party, ambavyo vimegura Azimio la Umoja One Kenya, vimemshawishi kuwa kisheria ni sehemu ya Muungano wa Ruto hivyo basi kwa ujumla Muungano huo unastahili kuwa Muungano wa Walio Wengi katika bunge hilo kwa wabunge 179 dhidi ya wabunge wa Azimio La Umoja One Kenya, 157.

Hivyo, kwa maamuzi hayo Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya ndio utakaokuwa wa Walio Wachache katika Bunge hilo.

Muungano wa Rais Ruto wateua kiongozi wa wengi bungeni

Hivyo, Wetang’ula amemtangaza rasmi Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung'wa kuwa kiongozi wa Walio Wengi, huku Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya akiwa naibu wake. Mbunge wa Mugirango Kusini, Silvanus Osoro atakuwa kiranja na kusaidiwa na Naomi Waqo.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandanyi atakuwa kiongozi wa Walio Wachache, na kusaidiwa na Robert Mbui, mbunge wa Kathiani.

Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed atakuwa kama Kiranja wake katika Bunge la 13 na kusaidiwa na Mbunge mteule Sabina Chege, kutokana na maamuzi hayo ambayo yanapingwa vikali na wabunge wanaogemea mrengo wa Odinga.

Muungano wa Odinga ulikuwa na wabunge wengi kabla ya baadhi ya wabunge kumtoroka na kujiunga na Ruto

Kabla ya makubaliano hayo ya kisiasa, yaliowafanya wabunge hao kugura, Odinga kupitia Muungano wake wa Azimio la Umoja One Kenya, alikuwa na idadi nyingi ya wabunge 171 dhidi ya wabunge 165 wa Kenya Kwanza.

Kutokana na Maamuzi ya Wetang’ula, Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge inayotwikwa majukumu ya upangaji wa shughuli zitakazofanywa na Bunge na mambo yote yanayohusiana na Kanuni za Kudumu za bunge, kuwapigia msasa walioteuliwa na Ruto kuwa mawaziri na nyadhifa nyingine, itaendelea na shughuli zake kwani suitafahamu hiyo ilikuwa inasambaratisha uwezekano wa kutekeleza shughuli hizo.

Kwa kawaida, shughuli ya kwanza katika kikao cha kwanza mwanzoni mwa muhula wa bunge huwa ni kubuniwa kwa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge lakini sasa kutokana na utata huu uliopo, bunge hilo limelazimika kujadili hotuba ya rais baada ya ufunguzi wa bunge la 13.

Imeyatarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi.

XS
SM
MD
LG