Serikali ya Ufaransa inaendelea na juhudi kali kuwasaka waliofanya mashambulizi ambayo Rais Francois Hollande amesema ni "kitendo cha vita" dhidi ya nchi yake, huku kukiwa na hofu kuwa waliofanya vitendo hivyo wanapanga mashambulizi mapya.
Kundi la Islamic State limedai kuhusika katika shambulizi hilo la Ijumaa Novemba 13, na kusababisha mauaji, hasira miongoni wafaransa na jumuiya ya kimataifa.
Hadi Jumamosi jioni idadi ya waliokufa ilitajwa kuwa watu wasiopungua 129.
- Watu 352 wamejeruhiwa, 99 wakiwa katika hali mbaya
- Magaidi 7 wameuawa, walikuwa katika timu za watu watatu watatu
- Walinzi wa usalama 1500 zaidi wa Ufaransa wameongezwa kwenye msako huo uliosambaa hadi Ubelgiji
Rais Hollande amelaumu kundi la IS ambalo limeshambulia nchi kadha katika juhudi zake za kuanzisha ukhalifa katika nchi za Syria na Iraq.
Lakini afisa wa kupambabana na ugaidi nchini Ufaransa anasema maafisa bado walikuwa wanaendelea kutafuta endapo washambuliaji waliokufa walikuwa wakazi wa Ufaransa na endapo wana wenzao wanaosubiri kushambulia tena. Ulinzi umeongezwa kote Ufaransa na katika mipaka ya nchi za jirani dhidi ya mashambulizi zaidi.