Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 02, 2024 Local time: 00:20

Mapigano yapamba moto Ivory Coast


Mapigano yanazidi kuongezeka huko Ivory Coast kati ya wafuasi wa Gbagbo na Ouattara, March 26,2011.
Mapigano yanazidi kuongezeka huko Ivory Coast kati ya wafuasi wa Gbagbo na Ouattara, March 26,2011.

Mapigano makali yamezuka katika mji wa Duekoue nchini Ivory Coast huku wafuasi wa marais wapinzani wanapigana kudhibiti eneo la magharibi mwa nchi.

Wakazi wa mjini humo wameripoti kusikia milipuko na silaha nzito zikifyatuliwa leo Jumatatu. Shirika la habari la Ufaransa-AFP, limesema wapiganaji wanaomuunga mkono Rais anayetambuliwa kimataifa Alassane Ouattara wanajaribu kuukamata mji.

Waasi wanaomuunga mkono Ouattara wameongeza udhibiti katika eneo la magharibi mwa Ivory Coast dhidi ya majeshi yanayomtii Rais Laurent Gbagbo anayeng’ang’ania madaraka. Wapiganaji wa kundi la New Forces wanasema wamekamata miji mitano kutoka kwa majeshi yanayomuunga mkono Gbagbo katika wiki za karibuni.

Bwana Gbagbo anakaidi wito wa kimataifa wa kukabidhi madaraka kwa amani kwa bwana Ouattara, ambaye Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika unamtambua kama mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika mwezi Novemba.

Mji wa Duekoue upo kwenye kwenye barabara inayoelekea Liberia upande wa magharibi au Guinea kwa upande wa Kaskazini.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa linasema hadi watu milioni moja wamekimbia nyumba zao kwa sababu ya ghasia za baada ya uchaguzi nchini Ivory Coast.

Umoja wa Mataifa unasema watu wasiopungua 462 wameuwawa katika ghasia hizo tangu mgogoro huo ulipoanza mwezi Disemba. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litabuni suluhisho wiki hii ambalo linapelekea kuweka vikwazo dhidi ya bwana Gbagbo na washauri wake wa karibu.

XS
SM
MD
LG