Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Julai 23, 2024 Local time: 17:06

UN yaongeza vikwazo kwa Eritrea


Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuongeza vikwazo dhidi ya Eritrea
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuongeza vikwazo dhidi ya Eritrea

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuongeza vikwazo dhidi ya Eritrea kwa kuendelea kuwasaidia wanamgambo wa al-Shabab

Eritrea inapinga azimio jipya la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linaweka vikwazo vikali dhidi ya nchi hiyo kwa kuwasaidia waasi nchini Somalia.

Taarifa kutoka wizara ya mambo ya nchi za nje ya Eritrea imesema jumanne kwamba azimio hilo litaongeza mivutano na kuchochea hali ya milipuko ambayo tayari ipo katika pembe ya Afrika.

Jumatatu, baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura 13 dhidi ya 0 kupitisha azimio hilo, ambapo China na Russia haikushiriki.

Azimio hilo linailaani Eritrea kwa kukiuka vikwazo vilivyowekwa mwaka 2009, kwa kuendelea kuwasaidia wanamgambo wa ki-Islam nchini Somalia, ikiwemo kundi la al-Shabab. Azimio pia linaruhusu baraza kuongeza idadi ya watu na nyadhifa zao ambao wanaweza kukabiliwa na vikwazo vinavyoweka marufuku ya safari na kuzuiliwa mali zao.

Eritrea inakanusha kuwasaidia al-Shabab na makundi mengine ya wanamgambo. Wizara ya mambo ya nchi za nje nchini humo ililaani vikwazo hivyo vipya vilivyoshinikizwa na Marekani dhidi ya Eritrea. Nchi hiyo ilisema vikwazo hivyo pia vinalenga kuilinda Ethiopia, ambaye ni mshirika wa Marekani katika mapigano dhidi ya ugaidi.

Mataifa haya mawili yaliopo Afrika mashariki yanapingana ambapo walipigana vita juu ya mpaka kati ya mwaka 1998 na 2000.

Jumatatu, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, alikuwa miongoni mwa viongozi kadhaa wa Afrika mashariki ambao waliliomba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo vikali dhidi ya Eritrea.

Eritrea tayari iliwekewa marufuku ya silaha na Umoja wa Mataifa kwa sababu ya shutuma zilizopo kuwa inawasaidia wanamgambo wa al-Shabab. Kundi hilo la wanamgambo wa ki-Islam linajaribu kuiangusha serikali ya mpito nchini Somalia na kuwa nchi ya ki-Islam.

XS
SM
MD
LG