Rais wa Tume ya ECOWAS, Jean Claude Kassi Brou amesema viongozi 15 wa Jumuia ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi wamekubaliana kukutana tena Julai 3 kabla ya kuamua juu ya kuziweka vikwazo nchi tatu zilizositishwa uanachama wake.
Hata hivyo baadhi ya maafisa waliohudhuria mkutano huo uliomalizika Jumamosi usiku mjini Accra, Ghana wanasema viongozi hao hawakuweza kukubaliana hasa kuhusiana na vikwazo dhidi ya Mali.
Kwa upande wake Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amewasihi viongozi wenzake kufikiria kwanza maisha ya raia wa kawaida watakaoathirika zaidi na vikwazo, kabla ya kuchukua hatua yoyote.
Taarifa ya ofisi yake inaeleza kwamba kiongozi huyo amesema kwamba tangu mkutano wa mwisho wa viongozi wa ECOWAS hakuna mafanikio muhimu yaliyopatikana kuhusiana na ratiba ya kuitisha uchaguzi na kurudisha utawala wa kidemokrasia huko Mali, Guinea na Burkina Faso.
Viongozi wa mapinduzi katika mataifa hayo matatu wametangaza kipindi cha mpito kuelekea demokrasia kirefu zaidi kuliko vile viongozi wa jumuia hiyo wangependa kuona.
Kwa upande wake, Kassi Brou ametoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuongeza misaada yao kwa Mali, na Burkina Faso ambako hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya kutokana na mambo kadhaa ikiwemo ukosefu wa usalama.
ECOWAS tayari tangu mwezi Januari imeiwekea Mali vikwazo vya kiuchumi na kusababisha biashara kusita kabisa kuingia na kutoka katika mataifa jirani.
Facebook Forum