Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 28, 2023 Local time: 09:23

Soko la Pamoja A. Mashariki laanza


Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zimezindua rasmi soko la pamoja la Afrika Mashariki leo Julai mosi.

Soko la pamoja la Afrika Mashariki limeanza rasmi leo Julai 1, 2010 kufuatia hatua ya wakuu wa nchi hizo wanachama za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kutia saini mkataba wa soko hilo Novemba mwaka jana mjini Arusha, Tanzania ambako ndio makao makuu ya jumuia hiyo.

Marais wa nchi hizo walikubaliana kuwepo kwa biashara huru na kuvuka kwa watu kutoka nchi moja hadi nyingine bila ya vizuizi katika eneo lote. Hata hivyo maafisa katika makao makuu ya jumuiya hiyo wamekiri kuwa maswala kadha bado yanahitaji kushughulikiwa mpaka mfumo huo ufanye kazi kama ilivyodhamiriwa. Inatarajiwa kuwa mkataba huu wa soko la pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki utaongeza ushawishi wa kiuchumi katika eneo hilo lenye watu wanaokadiriwa kufikia milioni mia moja na 30.

Hatua hii inakuja miaka 33 tangu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki hapo mwaka 1977 – ambayo ilikuwa ikishirikisha nchi za Tanzania, kenya na uganda. Chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mataifa hayo matatu yalikuwa na taasisi za pamoja kama vile shirika la ndege la Afrika Mashariki, shirika la Posta na Simu, na shirika moja la Bandari. Jumuiya hiyo ilivunjika hasa kutokana na tofauti za kisiasa.

Kuanzishwa kwa soko la pamoja ni hatua ya pili muhimu baada ya ile ya ushuru wa forodha ambayo inatarajiwa kupanua wigo wa masuala ya ushirikiano kwa kujumuisha nyenzo za uzalishaji na biashara ya huduma. Soko la pamoja ni ngazi ya ushirikiano ambayo si tu katika sekta ya uchumi bali pia masuala ya kijamii na siasa.

XS
SM
MD
LG