Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Julai 25, 2024 Local time: 16:01

maelfu ya watu wamepoteza maisha kutokana na njaa Afrika mashariki


Watoto katika baadhi ya maeneo yaliyokumwa na njaa Afrika mashariki
Watoto katika baadhi ya maeneo yaliyokumwa na njaa Afrika mashariki

Jumuiya ya kimataifa inalaumiwa kwa kuchukua hatua za taratibu kuepuka mzozo wa njaa Afrika mashariki

Mashirika ya misaada yanasema maelfu ya watu walipoteza maisha yao kutokana na mzozo wa chakula huko Afrika mashariki kwa sababu jumuiya ya kimataifa ilichukua muda mrefu kusaidia hadi pale ukosefu wa chakula ulipogeuka kuwa mzozo wa dharura.

Ripoti iliyotolewa Jumatano na shirika la Oxfam na Save the Children imesema tatizo la ukosefu wa chakula lilitangazwa mapema tangu mwezi Agosti 2010, lakini mataifa tajiri wahisani yalishindwa kufanya chochote mpaka njaa ilipotangazwa katika maeneo ya Somalia mwaka 2011.

Mkuu wa Oxfam, Barbara Stocking, alisema katika taarifa kwamba, kutaabika kwa maelfu ya watoto kungeweza kuzuiliwa kama jumuiya ya kimataifa ingesaidia wakati ishara za kwanza za njaa zilipojitokeza.

Ripoti inasema haitowezekana kujua idadi ya watu waliopoteza maisha kwa sababu ya ukame, lakini inainukuu serikali ya Uingereza ikisema kati ya watu 50,000 na 100,000 wamekufa kati ya mwezi April na Agosti mwaka 2011. Ripoti inasema zaidi ya nusu ya vifo hivyo vilikuwa vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na wengi wao walikuwa wasomali.

Ripoti pia inasema kwamba kusafirisha kwa dharura maji kwenye maeneo yaliyoathirika inagharimu zaidi ya mara tatu ya dola 900,000 ambayo ingeliweza kugharimia kutengeneza vyanzo vya maji katika kanda kwa ajili ya msimu ujao wa ukame.

Ripoti hiyo inaihimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka zaidi kuepuka janga katika nchi za Afrika Magharibi, ambako inasema tatizo la ukosefu wa chakula limeanza kujitokeza na kutishia kuathiri maisha ya mamilioni ya watu.


XS
SM
MD
LG