Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Februari 06, 2023 Local time: 23:05

DRC yaishtumu Rwanda kuunga mkono waasi wa M23


Wanajeshi wa Congo wanawaomba raia kurudi majumbani mwao kufuatia mapigano na waasi wa M23 eneo la Kanyamahoro, May 25, 2022. Picha ya AFP

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeishtumu Rwanda kuunga mkono kundi la waasi la M23, jambo ambalo Rwanda imekanusha Alhamisi wakati jeshi la Congo likipambana na waasi hao katika eneo la mashariki mwa nchi.

Mapigano na kundi hilo la waasi yalizuka kwenye maeneo mengi wiki hii katika mkoa wa Kivu Kaskazini unaopakana na Rwanda.

“Tuhuma zinaonyesha kuwa M23 ilipata uungwaji mkono wa Rwanda,” msemaji wa serikali ya Congo Patrick Muyaya alisema Jumatano jioni, baada ya mkutano wa dharura na waziri mkuu.

M23 ni moja ya zaidi ya makundi 120 yenye silaha ambayo yanapatikana mashariki mwa DRC.

Kundi hilo liliwahi kuuteka kwa muda mfupi mji wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma mwishoni mwa mwaka wa 2012, kabla ya jeshi kutokomeza uasi mwaka uliofuata.

Lakini M23 ilianzisha tena mapigano mwaka huu, ikiishtumu serikali ya Congo kushindwa kuheshimu makubaliano ya mwaka wa 2009 ambayo yalieleza kuwa wapiganaji wake wangepaswa kujumuishwa katika jeshi la taifa.

Waziri wa mambo ya nje wa DRC Christophe Lutundula ameiishtumu pia Rwanda kuwasaidia waasi wa M23 akisema kwamba, kundi hilo la waasi lilishambulia kambi ya kijeshi ya Rumangabo, umbali wa kilomita 40 kaskazini mwa Goma.

Lakini Rwanda imekanusha kuhusika katika mzozo huo kati ya M23 na serikali ya Congo. Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo amesema nchi yake “haina nia ya kuingizwa katika suala la ndani la DRC”.

Mapigano kati ya jeshi la Congo na M23 yaliendelea Alhamisi karibu na kambi ya Rumangabo, vyanzo vya eneo hilo vimesema.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG