Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 17:21

DRC yadai karibu kuwamaliza CNDP


Bosco Ntaganda, kiongozi wa kundi la uasi la CNDP nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC
Bosco Ntaganda, kiongozi wa kundi la uasi la CNDP nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC

Wanajeshi wa CNDP waliingizwa katika jeshi la taifa mwaka 2009 lakini mwaka huu walianza kuasi wakidai hali mbaya na mishahara midogo

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC- inasema inakaribia kulimaliza kundi la uasi la wanajeshi wanaomtii Bosco Ntaganda, kiongozi wa kijeshi anayetafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC.

Waziri wa Habari wa DRC, Lambert Mende, ameiambia Sauti ya Amerika-VOA, Jumatano kwamba jeshi limepiga hatua kubwa na linakaribia kulisambaratisha kundi hilo la uasi.

“Jeshi limepiga hatua na linafavya vyema. Ninafikiri sehemu kubwa sana za milima ambapo waasi hawa wanajificha zimechukuliwa tena na jeshi na tunamatumaini kwamba katika saa kadhaa au siku kadhaa zijazo kazi itakamilika”.

Ntaganda ambaye anajulikana kama “Terminator” anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC kwa shutuma za kutoa mafunzo na kuwatumia wanajeshi watoto katika jimbo la Ituri nchini DRC.

Wanajeshi wa kundi lake la CNDP waliingizwa katika jeshi la taifa mwaka 2009 lakini mapema mwaka huu walianza kuasi wakidai hali mbaya na mishahara midogo baada ya serikali ya DRC kutishia kumkamata kiongozi wao.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Luis Moreno-Ocampo alitangaza mwezi uliopita kwamba anafungua mashtaka mapya ya uhalifu wa vita dhidi ya Ntaganda ambaye yupo mafichoni.

Ocampo alisema anataka kuongeza mashtaka ambayo yanajumuisha uhalifu dhidi ya binadamu na mashambulizi ya kimataifa dhidi ya raia.

Mwezi Machi ICC ilimkuta na hatia mshirika wa zamani wa Ntaganda, Thomas Lubanga ya mashtaka ya kuwatumia wanajeshi watoto. Anakabiliwa na hukumu ya juu ya kifungo cha maisha jela.

Mapigano kati ya jeshi na waasi wanaoongozwa na Ntaganda yalizuka katika jimbo la Kivu Kaskazini mwishoni mwa mwezi April.

XS
SM
MD
LG