Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Agosti 03, 2021 Local time: 17:42

DRC: Tshisekedi apanga mikakati ya kumuondoa waziri mkuu na kumaliza kabisa ushirikiano na Kabila


Rais wa DRC Felix Tshisekedi

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi ameomba maseneta waliokaribu naye kuunda kundi la maseneta na wabunge wanaoweza kumsaidia kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri linalotawaliwa na watu wanaomuunga mkono aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila.

Tshisekedi alivunja mkataba wa kugawana madaraka na Kabila, mnamo mwezi Desemba.

Kabila aliondoka madarakani Januari mwaka 2019 baada ya kutawala Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kwa mda wa miaka 18 lakini watu walio karibu naye bado wanadhibiti bunge.

Rais Tshisekedi amesema kwamba mgawanyiko katika muungano wake na Kabila, umekwamisha juhudi zake za kumaliza mashambulizi ya makundi ya waasi mashariki mwa Congo, kulipo na utajiri mkubwa wa madini, kufanya mabadiliko katika mfumo wa mahakama, Pamoja na kupata ufadhili kutoka shirika la fedha duniani IMF Pamoja na benki kuu ya dunia.

Viongozi wanaomuunga mkono rais Tshisekedi katika bunge la nchi hiyo, walipiga kura Desemba tarehe 10 na kumuondoa spika wa bunge hilo, ambae ni mshirika mkubwa wa Joseph Kabila.

Tshisekedi amemteua seneta Modeste Bahati kusimamia shughuli ya kuhakikisha kwamba muungano wa seneta wanaomuunga mkono una wafuasi wengi kusaidia katika kutekeleza lengo lake.

Iwapo Tshisekedi atafaulu kupata idadi kubwa ya maseneta, bunge litakuwa na uwezo wa kuwasilisha mswada wa kutokuwa na Imani na serikali ya waziri mkuu Sylvestre Ilunga, ambaye ni mshirika mkuu wa Joseph Kabila.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG