Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 07, 2022 Local time: 10:23

Baadhi ya wafungwa waliotoroka DRC warudi wenyewe gerezani


Wafungwa walitoroka katika gereza la mjini Beni Jumanne alfajiri

Wafungwa waliorudi wamewaambia maafisa kwamba walilazimishwa kutoroka na wanapendelea kuendelea kukaa gerezani badala ya kuishi na waasi. 

Wafungwa 20 kati ya 1,300 waliotoroka gerezani katika mji wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wamerudi gerezani muda mfupi baada ya kutoroka.

Wafungwa waliorudi wamewaambia maafisa kwamba wanapendelea kuendelea kukaa gerezani badala ya kuishi na waasi.

Kulingana na Meya wa mji wa Beni Modeste Bakwanamaha, wafungwa waliorudi wamesema kwamba “walichukuliwa kwa nguvu na kwamba wamewatoroka waasi wa Allied Democratic Forces –ADF - waliowateka nyara baada ya kuvunja gereza jumanne asubuhi.”

Watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki, wanaoaminika kuwa wapiganaji wa kundi la ADF walivamia gereza la Kangbayi, mjini Beni na kuachilia huru zaidi ya wafungwa 1,300. Wafungwa 100 pekee walisalia gerezani.

Kulingana na Meya Bakwanamaha, “washambuliaji walikuwa wengi na walifanikiwa kuvunja milango ya gereza kwa kutumia machine za wahunzi zinazotumia umeme.”

Waasi wa ADF wadaiwa kuhusika

Hakuna kundi limedai kuhusika na uvamizi huo lakini meya Bakwanamaha anasema kwamba “tunaamini ni kundi la ADF lililofanya haya.”

Wafungwa wawili walipigwa risasi na kuuawa wakati wa tukio hilo la Jumanne saa kumi na nusu asubuhi, saa za Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo – DRC.

Meya Bakwanamaha amesema kwamba msako mkali unaoongozwa na jeshi la DRC unaendelea kuwatafuta wafungwa waliotoroka huku raia wakiwa wametakiwa kutoa ripoti zozote zitakazosaidia kukamatwa kwao.

Kundi la ADF limekuwa nchini DRC tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya kufurushwa Uganda.

Kulingana na umoja wa mataifa, kundi hilo limeua zaidi a watu 1,000 tangu mwanzoni mwa mwaka 2019 licha ya kuwepo msako wa maafisa wa jeshi la DRC.

Idadi kubwa ya wafungwa katika gereza la Kangbayi ni wanachama wa makundi ya waasi ikiwemo ADF.

Grereza hilo liliwahi kushambuliwa na waasi mwezi Juni mwaka 2017 na zaidi ya wafungwa 1300 kutoroka.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG