Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Julai 24, 2024 Local time: 20:35

Upinzani DRC watofautiana juu ya wabunge kushiriki katika vikao


Mgogoro wote huu wa kisiasa unaoendelea nchini DRC unatokana na uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 28, mwaka jana
Mgogoro wote huu wa kisiasa unaoendelea nchini DRC unatokana na uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 28, mwaka jana

Baadhi ya wabunge wa UDPS wanaona ni jambo la busara kushiriki katika vikao vya bunge ili kuwawakilisha watu wao huku uongozi ukitishia kuwaengua uanachama

Wabunge 17 wa chama cha upinzani cha UDPS nchini Burundi na washirika wao wamechukua hatua kwa hiari yao wenyewe ya kushiriki kwenye vikao vya bunge, lakini uongozi wa chama cha UDPS unasema kwamba mbunge yeyote atakae shiriki kwenye vikao vya bunge atatengwa kutoka chama hicho.

Wabunge hao wa chama cha UDPS wamesema hatua yao hiyo inalenga kuhakikisha kwamba haki ya raia waliowachagua imeheshimika. Hata hivyo wabunge wa chama cha UDPS na wale wa Dynamique Tshisekedi President- DTP,wanahisi kwamba kushiriki kwao bungeni hakuwapi uhalali, Rais Kabila na wabunge wa chama chake.

Mbunge wa UDPS, Kalonji Mukendi kutoka Kassaï-Oriental amesema licha ya kuja kwao bungeni, lakini wataendelea na msimamo wao wa kulazimisha kuwepo uhalali wa madaraka nchini hapa.“Tunataka kuwahakikishia wananchi wenzetu kwamba, tuko makini kwamba bunge hili limejaa na watu waliotajwa na tume ya uchaguzi na ambao kweli hawakuchaguliwa na raia. Nikinyume na maadili ya chama chetu cha UDPS. Lakini hatuwezi kususia vikao vya bunge ili kuwapa nafasi viongozi wa hivi sasa katika kuendelea na kuongoza kwa ajili ya maslahi yao binafsi”.

Uongozi wa chama cha UDPS umesema kwamba haukuwaruhusu wabunge hao kushiriki kwenye vikao vya bunge, na yeyote atakayejaribu kufanya hivyo basi ataondolewa kutoka ndani ya chama. Raymond Kahungu Mbemba ,naibu katibu mkuu wa chama cha UDPS ameiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba hatua ya kuondolewa kwa wabunge hao sio ya Etienne Tshisekedi, bali ya uongozi wa chama cha UDPS.

Duru zinaeleza kwamba tofauti imezuka ndani ya chama cha UDPS. Upande mmoja wamependekeza kwamba wabunge 41 wa chama hicho washiriki kwenye vikao vya bunge, huku upande mwengine wakishikilia kwamba kushiriki kwa wabunge hao ni kuhalalisha utawala wa Rais Joseph Kabila.

Mratibu wa vuguvugu la vyama vilivyomuunga mkono mgombea Etienne Tshisekedi wakati wa uchaguzi, Franck Diongo, alisema kuja kwao bungeni kunalenga kuomba uchaguzi urejewe:“Rais Tshisekedi,amekwisha futa uchaguzi wa bunge, inamaanisha kwamba mimi Franck Diongo nimefuata msimamo huo wa kubatilishwa kwa uchaguzi wa bunge na niko hapa ili kulazimisha kurejewa kwa uchaguzi wa Rais na wa bunge”.

Wakati huo huo wabunge wameunda tume ya pamoja ya bunge itakayotunga taratibu za ndani za bunge kabla ya uchaguzi wa sekretarieti ya kudumu ya baraza hilo.Tume hiyo imejumuisha wabunge 55 kutoka majimbo yote 11 ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC.
XS
SM
MD
LG