Tume ya uchaguzi nchini Congo imemtangaza Rais Joseph Kabila kuwa mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika wiki iliyopita.
Tume ya uchaguzi ilitangaza mjini Kinshasa Ijumaa jioni kuwa Rais Kabila ameshinda kwa kupata asilimia 49 ya kura zote ikilinganishwa na asilimia 32 alizopata mpinzani wake wa karibu Etienne Tshisekedi wa chama cha UDPS. Matokeo hayo ni lazima yaidhinishwe na mahakama kuu ya DRC
Mara baada ya tangazo hilo mpinzani Etienne Tshisekedi alisema anapinga matokeo ya uchaguzi na badala yake akijitangaza mwenyewe kuwa ni rais wa nchi hiyo.
Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, Tshisekedi alisema anaona matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi nchini Congo kuwa ya uwongo. Bwana Tshesekedi alisema “umeyasikia matamshi kutoka kwa M.Ngoy Mulunda rais wa tume ya uchaguzi. Matamshi hayo yanaenda kinyume dhidi ya watu wetu. Siyatambui”
Alisema kwamba binafsi anaona kadri siku zinavyokwenda kuwa yeye ni Rais aliyechaguliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tshisekedi alitaka kila mtu kuwa mtulivu hadi atakapotoa maelezo zaidi. “Ninaisihi jumuiya ya kimataifa ambayo imerudia tena kunitaka kufanya taratibu za kisiasa kwa amani, kuingilia kati ili kuiepusha Congo kuingia katika umwagaji damu mpya katika eneo.”
Naye mgombea mwingine wa upinzani nchini DRC, Vital Kamerhe, anasema anapinga matokeo hayo na kwa upande wake “Etienne Tshisekedi ndiye Rais aliyechaguliwa”.
Baada ya matokeo kutangazwa mwandishi wa Sauti ya Amerika Scott Stearns, aliripoti kuona matairi yakichomwa moto jirani na Kinshasa kwa wafuasi wa bwana Tshisekedi, japokuwa hakukuonekana kuwepo ghasia.
Kabla ya matokeo kutangazwa, vyama vya upinzani viliwashutumu maafisa wa uchaguzi kuhusu wizi wa kura na walionya kufanya maandamano makubwa na uwezekano wa kutokea ghasia.
Majeshi ya usalama yamejiandaa vyema iwapo kutatokea ghasia na Umoja wa Mataifa, Marekani, Umoja wa ulaya na Umoja wa Afrika unasisitiza kuwepo hali ya utulivu kwa wananchi.
Tume ya uchaguzi nchini Congo ilichelewa kutangaza matokeo rasmi kwa siku tatu, ikidai kuwepo matatizo ya kimsingi.