Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 10:32

DRC: Wanajeshi wa Uganda na Congo wameongeza mashambulizi dhidi ya waasi wa ADF


Wanajeshi wa DRC, wanaoshirikiana na wanajeshi wa Uganda kupambana na kundi la waasi la ADF mashariki mwa Congo. PICHA: AFP
Wanajeshi wa DRC, wanaoshirikiana na wanajeshi wa Uganda kupambana na kundi la waasi la ADF mashariki mwa Congo. PICHA: AFP

Jeshi la Uganda UPDF limeongeza mashambulizi dhidi ya waasi wa kundi la kiislamu la allied democratic forces - ADF, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Roketi na mizinga mizito inaendelea kufyatuliwa, ikilenga kambi za ADF baada ya taarifa za ujasusi kwamba waasi wa ADF wamekuwa wamejikusanya na kuunda kambi kadhaa kivu kaskazini.

Oparesheni ya jeshi la Uganda nchini DRC kwa jina Shujaa, ilianza Novemba mwaka uliopita, lakini ilisitishwa kwa mda baada ya ruhusa ya serikali ya DRC kumalizika mwezi mwezi May kabla ya DRC kuingia na Uganda makubaliano mapya.

Jumla ya wanajeshi 1700 wa Uganda wanaendeleza oparesheni hiyo nchini Congo.

Ngome za waasi wa ADF

Maafisa wa usalama wa Uganda wanaamini kwamba waasi wa ADF wamaimarisha shughuli zao karibu na mto Lisulubi, kusini mwa mpaka wa Busunga, kwenye barabara ya Semuliki. Waasi hao pia wanaminika kukimbilia sehemu za Maraud, Mwalika, Mwenda, Mutwanga na katika mbuga ya kitaifa ya Wanyama ya Virunga.

Kabla ya oparesheni hiyo kusitishwa, waasi hao walikuwa wametawanyika kote Kivu kaskazini kutokana na mashambulizi ya jeshi la Uganda UPDF, kwa ushirikiano na jeshi la DRC.

Patrick Munduga, ni mkurugenzi wa shirika la Ark, linalofuatilia shughuli za kundi la waasi la ADF.

“Hii sio vita ambavyo vinaweza kufaulu kwa njia moja tu ya kurusha mabomu na kupiga risasi. Hii ni vita ya kushirikisha raia. Wapiganaji wa ADF hawakai sehemu moja. Kutokana na misitu ya Congo inakuwa vigumu kwa wanajeshi kuwapiga adui ambao hawana uhakika mahali wamejificha.”

Mbinu za jeshi la Uganda

Kwa kawaida, jeshi la Uganda hutumia sana mashambulizi ya angani na ya roketi za masafa marefu kabla ya wanajeshi wake wa nchi kavu kuingia katika sehemu za vita.

Kabla ya kuanza oparesheni hiyo mwezi Novemba mwaka uliopita, jeshi la Uganda lilitangulia kurusha makombora ndani ya DRC, kutoka Uganda. Oparesheni hiyo ilifanikiwa kuwasukuma nyuma waasi wa ADF, kabla ya wanajeshi hao kuingia nchini humo kwa oparesheni maalum.

Waasi wa ADF wameripotiwa kuvamia vijiji kaskazini mwa Kivu na kuua watu 24, sehemu za Mamove na Beni-Kasindi, karibu na mpaka wa DRC na Uganda.

Kulingana na mkataba wa awali kati ya serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Uganda, oparesheni shujaa, dhidi ya waasi wa ADF ilipangiwa kumaliza ndani ya miezi sita, kati ya mwezi Nobemba mwaka uliopita 2021, na April mwaka huu 2022. Oparesheni hiyo iliongezewa mda baada ya tathmini za kiusalama.

Patrick Munduga, mkurugenzi wa shirika na anchor, anasema kwamba kutokana na mazingira magumu ya kufanya kazi kwa wanajeshi oparesheni hiyo itachukua mda mrefu.

“Vita dhidi ya kundi la ADF haviwezi kumalizika saa hii. Jeshi la Uganda lilifanikiwa kufukuza waasi wa Lord’s resistance Army LRA, kwa sababu waliwashirikisha wananchi. Watu katika sehemu wapiganaji walikuwa, walikuwa wanatoa Habari kwa wanajeshi na vyombo vya Habari vilitumika sana kutoa taarifa kwa watu. Nchini Congo, vita dhidi ya ADF, raia wanakimbia tu bila kutoa ripoti kwa jeshi, na wanajeshi wanarusha makombora bila kushirikiana na raia.”

Jeshi la jumuiya ya Afrika mashariki

Viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki wanaendelea kuweka mikakati ya kutuma wanajeshi wake nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kupambana na makundi ya waasi baada ya kundi la M23, linaloongozwa na Generali Sultan Makenga, kuongeza mashambulizi na kudhibithi mji muhimu wa Bunagana kutoka kwa wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Raia wa DRC hata hivyo hawana Imani na namna jeshi la Jumuiya ya Afrika mashariki litakalofanya kazi, na iwapo lina nguvu za kuangamiza Zaidi ya makundi ya waasi 120 yanayoripotiwa kuwa mashariki mwa Congo.

Museveni anaendelea na miradi ya barabara na biashara ndani ya DRC

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ameonyesha matumaini ya kupatikana amani mashariki mwa DRC na biashara kati ya nchi hiyo na Uganda kunawiri pakubwa.

Katika kikao na wakurugenzi wa kampuni kubwa za kibiashara nchini Uganda, uliofanyika nyumbani kwake Irenga, wilayani Ntungamo, Museveni amesema kwamba Uganda itajenga barabara kadhaa ndani ya DRC, ambazo watumiaji watakuwa wanalipia, ili kuimarisha biashara kati ya Uganda na DRC.

Kwa sasa Uganda inagharamia ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 223. Ujenzi unasimamiwa na kampuni ya ujenzi nchini Uganda, Dott services, ambayo umiliki wake umehusishwa na ndugu ya Museveni, Caleb Akwandanaho, maarufu kama Salim Saleh.

Museveni anaamini kwamba barabara anazojenga ndani ya DRC, zitaimarisha biashara kati ya miji ya Beni, Goma na Butembo.

Ameahidi kuwasaidia wafanyabiashara wa Uganda kifedha, kuimarisha biashara kati ya DRC na Uganda.

Hatua hii, imepelekea mjadala ndani ya Uganda, iwapo Oparesheni ya jeshi la Uganda ndani ya DRC ni ya maslahi ya kiusalama ama ya kibiashara.

Museveni pia ameahidi kuhakikisha kwamba shirika la Habari la Uganda, UBC, linaongeza uwezo wake wa kufika mbali na kusikika na kutazamwa kote mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Uganda pia itakuwa na mjumbe maalum wa kibiashara, mwenye uwezo wa kuzungumza lugha mbalimbali kuakilisha maslahi ya Uganda ndani ya DRC.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG