Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 05, 2024 Local time: 08:18

DRC yakabidhi vijana zaidi ya 100 kwa serikali ya Burundi


Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) Jumanne iliwakabidhi kwa serikali ya Burundi vijana zaidi ya mia moja iliyokuwa ikiwashikilia katika magereza yake.

Gavana wa Kivu Kusini, Marcelin Chishambo alikanusha taarifa kuwa vijana hao ambao ni raia wa Burundi walikuwa wapiganaji.

Amesema vijana hao walikuwa wakizuiliwa katika magereza mbali mbali kwa zaidi ya mwaka mmoja katika jimbo hilo

Lakini amesema baadhi yao walikutwa na nyaraka za kuomba hifadhi nchini Rwanda wakati wakiwa kwenye ardhi ya DRC na hivyo kuchukuliwa kama wahamiaji haramu.

Vijana 124 wa Burundi waorodheshwa

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA Bujumbura ameripoti kuwa kwenye mpaka baina ya Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, maafisa wa usalama waliorodhesha majina ya watu hao ambao walikuwa chini ya ulinzi mkali.

Amesema vijana hao walipandishwa katika lori wakiwa njiani kuelekea jijini Bujumbura.

Vyanzo vya habari vinasema kuwa vijana hao ambao ni raia wa Burundi walikuwa gerezani nchini Kongo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliwatia mbaroni baada ya kuwakuta hawana vibali vya kuishi nchini humo.

Zoezi limesimamiwa na maafisa wa pande mbili

Hata hivyo mwandishi wetu amesema kuwa zoezi hili limesimamiwa na maafisa mbali mbali wa nchi hizo mbili.

Huko Mkoa wa Kivu Kusini afisa mwandamizi, Charles Frispi wa ofisi ya MONUSCO amesema: “Tuko hapa kufuatilia zoezi hili, tuhakikishe haki za binadamu zinaheshimiwa na pia kuona kuwa viongozi walioko hapa wanafuata sheria na kulinda haki za raia.

Kwa jumla wote ni vijana 124 ambapo wawili kati yao wamelazwa katika hospitali ya mjini Uvira, amesema Gavana wa mkoa wa Kivu Kusini.

Ameongeza kuwa wanasubiriwa wapone ili wawahoji iwapo wanataka kurejea nchini Burundi au la.

Kwa mujibu wa Gavana kuna warundi 35 katika kundi hilo la vijana ambao walikataa kurejeshwa Burundi wakihofia usalama wao.

Waziri wa Burundi atoa tamko

Waziri wa Sheria wa Burundi aliyekuwa mpakani tayari kuwapokea warundi hao alisema ni haki yao kufanya uamuzi kubakia au kuondoka DRC.

Lakini alitoa wito kuwa warejee nyumbani kwani haoni sababu ya msingi inayowazuia kurejea makwao.

Waziri aliongeza: “Hakuna tatizo, Burundi ni nchi yao, ndio sababu tumekuja kuanzia asubuhi ili kuwapokeya, tunataka wajisikie kama wako katika nchi yao inayowajali.

Alisema watahifadhiwa katika eneo salama ili wahojiwe kwanza zijulikane sababu zilizowapelekea kwenda nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na baadaye wakikutikana bila hatia watakabidhiwa familia zao.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Haidallah Hakizimana, DRC

XS
SM
MD
LG