Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 20, 2024 Local time: 11:39

Dk. Ulimboka apigwa na watu wasiojulikana .


wagonjwa walowasilishwa hospitali ya Muhimbili na kulazwa chini kutokana na ukosefu wa huduma kutokana na mgomo wa madaktari.
wagonjwa walowasilishwa hospitali ya Muhimbili na kulazwa chini kutokana na ukosefu wa huduma kutokana na mgomo wa madaktari.

Dk. Namala Mkopi , amesema Dk. Ulimboka alipigiwa simu na watu ambao walimteka na kumpeleka Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam ambako alipigwa na kupoteza fahamu.

Hali ya kutoeleweka imeibuka leo nchini Tanzania baada ya tukio la kutekwa na kujeruhiwa vibaya kwa mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari Tanzania, walio katika mgomo, Dakta Steven Ulimboka.

Sauti ya Amerika imeshuhudia gari la wagonjwa lililombeba Dkt Steven Ulimboka likiingia katika hospitali ya taifa ya Muhimbili na hatimaye pilika pilika za kuokoa maisha yake kuanza huku akionekana akiwa katika hali mbaya.

Akizungumza mara ya baada ya Dk. Ulimboka kupatiwa huduma ya kwanza, rais wa chama cha madaktari Tanzania (MAT) Dk. Namala Mkopi , amesema Dk. Ulimboka alipigiwa simu na watu ambao walimteka na kumpeleka katika pori moja eneo la pande nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam ambako alipigwa na kupoteza fahamu mpaka wasamaria wema walipomkuta majira ya asubuhi akiwa katika hali mbaya na kumpeleka katika kituo cha polisi ambacho hakikutajwa jina.

Dk.Mkopi amelaani kitendo hicho na kukiita ni cha kinyama na pia kimewavunja moyo madaktari wote na kuwafadhaisha lakini pia kimeondoa moyo wa huruma kwa madaktari ambao wamesema wanadai haki yao ya msingi.

Nao wanaharakati wa haki za binadamu wanaitaka serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo la kujeruhiwa kwa Dk. Ulimboka lililoibua hisia tofauti miongoni mwa watanzania.

Hellen Kijo Bisimba Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu alikuwepo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili amesema serikali inapaswa kuwaridhisha watanzania kwamba haihusiki na tukio hilo kwa kuunda tume huru ya uchunguzi kubaini ukweli wa kutekwa na kupigwa kwa Dk. Ulimboka

Katibu wa jumuiya ya madaktari Tanzania Edwin Chitage amesema kujeruhiwa kwa kiongozi wao imekuwa kama chachu ya kuendelea kutetea haki zao kwa gharama yoyote!

Kwa upande wake Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam Suleman Kova katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema polisi wameanza uchunguzi wakina juu ya kutafuta watu waliohusika katika tukio hilo na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika.

Kamanda Kova alikanusha dhana ambayo kwasasa imejaa vichwani na watanzania walio wengi kwamba tukio hilo limefanywa na wanausalama, huku akitaka raia wema kusaidia katika uchunguzi huo.

Kutoka Dodoma, Serikali imeliahidi bunge kutoa kauli juu ya hatua ambazo itazichukua dhidi ya madaktari hapo Alhamisi, baada ya juhudi zote za kumaliza mgomo dhidi ya madaktari kushindikana.

Ahadi hiyo ya serikali imetolewa na Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda mbele ya bunge, kufuatia naibu spika wa bunge Bw. Job Ndugai kuombwa muongozo na mbunge wa Mbozi Mashariki, Bw. Godfrey Zambi, kuhusiana na mgomo huo wa madaktari.


XS
SM
MD
LG