Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Septemba 16, 2024 Local time: 00:20

Mkusanyiko wa habari kuhusu Covid-19 barani Afrika


Mhudumu wa afya anamfanyia vipimo mwanamke kubaini kama ameambukizwa virusi vya Corona.
Mhudumu wa afya anamfanyia vipimo mwanamke kubaini kama ameambukizwa virusi vya Corona.

Bunge la Kenya lilifanya kikao maalum Jumanne na kujadili mapendekezo yaliyopitishwa na baraza la mawaziri kuhusu jinsi ya kukabiliana na athari zinazojitokeza kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona. 

Ni wabunge 53 tu kati ya wote 349 walioruhusiwa kuwepo ndani ya bunge kwa mjadala huo kwa kuzingatia ushauri wa afya.

Kati yao ni kiongozi wa walio wengi bungeni, viranja wa vyama na viongozi wa kamati mbalimbali za bunge.

Nchini Burundi, shirikisho la mpira limepiga marufuku mechi zote za mpira nchini humo, wiki mbili baada ya kuripoti kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya Corona.

Shirikisho hilo lilisema awali halitafuta michezo na badala yake kudai kwamba lilikuwa limeweka mikakati ya kutosha kuwalinda wachezaji dhidi ya maambukizi.

Lilieleza kuwa inawezekana kuwasilisha washiriki katika mashindano ya kimataifa, kabla ya siku ya mwisho ya Mei 30.

Kufikia sasa, Burundi imeripoti visa 5 vya maambukizi ya Corona.

Nchini Sudan, shughuli za kawaida zitasitishwa kwa muda wa wiki tatu katika mji mkuu wa Khartoum, kuanzia Jumamosi hii, ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Msemaji wa serikali Faisal Salih alisema amri ya watu kusalia makwao pia itahusisha mji wa Omdurman.

Watu wataruhusiwa tu kununua bidhaa muhimu kama chakula na dawa, na kwa muda maalum.

Sudan imeripoti maambukizi ya watu 29 na vifo 4 kutokana na Corona.

Afrika kusini nayo imesema inafanikiwa katika vita dhidi ya virusi vya Corona kutokana na amri ya watu kusalia makwao. Maambukizi yanaripotiwa kupungua nchini humo.

Katika hotuba iliyoonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya taifa, mwenyekiti wa kamati ya serikali kupambana na Corona Prof Abdool Karim, alisema kuna mafanikio katika kudhibiti kiwango cha maambukizi mapya.

Afrika kusini imesema imepata mafanikio ya kipekee na kwamba hakuna nchi imefanikiwa kupunguza idadi ya maambukizi kwa haraka, jinsi iilivyofanya.

Prof Abdool alisema kuchukua hatua za haraka, na kuamurisha watu kukaa majumbani kulisaidia sana kukabiliana na virusi vya Corona kusambaa nchini humo.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, ameamrisha kuongezewa kwa muda wa watu kutotoka makwao kwa siku zingine14 baada ya siku 14 zilizowekwa awali kumalizika.

Amri hiyo inatekelezwa katika majimbo ya Abuja, Lagos na Ogun.

Wafanyakazi muhimu zaidi, maduka ya chakula na ya dawa pekee ndiyo yanaruhusiwa kufunguliwa.

Kwingineko shirika la fedha duniani IMF, limesimamisha kwa muda ulipaji wa madeni kwa nchi 19 za Afrika kwa muda wa miezi sita, ili kuziruhusu kutumia pesa hizo katika kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Nchi hizo ni Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Comoros, Burkina Faso, Chad, Afrika ya kati, Msumbiji, Benin, na Gambia. Zingine ni Guinea Bissau, Liberia, Madagascar, Malawi, Mali, Niger, São Tomé and Príncipe, Sierra Leone na Togo.

-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG