Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 03:03

Daktari nchini DRC apewa tuzo kwa kuwahudumia waathirika wa ubakaji


Baadhi ya wanawake kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC, nchi ambayo wanawake wengi ni waathirika wa ubakaji.
Baadhi ya wanawake kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC, nchi ambayo wanawake wengi ni waathirika wa ubakaji.

Daktari mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, amepokea tuzo kutoka taasisi moja ya Ubelgiji, kwa kazi yake ya kuwasaidia wanawake ambao wamebakwa.

Denis Mukwege, Daktari bingwa wa masuala ya wanawake, ametunukiwa tuzo ya kimataifa inayojulikana kama King Baudouin International Development mjini Brussels jana Jumanne. Mukwege, alianzisha hospitali moja huko mashariki mwa Congo katika mji wa Bukavu, kwa kutoa huduma za bure kwa waathirika wa ghasia za ngono.

Taasisi binafsi ya King Baudouin, ambayo ilitoa tuzo hiyo, iliisifia hospitali ya Mukwege kwa kutoa huduma zote za kiafya na ushauri wa kiakili kwa kuwasaidia waathirika kuondokana na mawazo ya ghasia za ngono. Taasisi inasema katika kipindi cha muongo uliopita, Mukwege na timu yake wamewahudumia zaidi ya watu 30,000.

Mukwege alisema ni heshima kwake kupewa tuzo hiyo na anashukuru kwa kupewa nafasi ya kuzungumza kuhusu umuhimu wa watu kuchukua hatua kuwasaidia wanawake huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mbali na tuzo hiyo pia atapokea fedha taslimu dola 200,000 . Tuzo hiyo ilianzishwa na taasisi ya King Baudouin zaidi ya miaka 30 iliyopita kuwatambua wote wanaofanya kazi kusukuma mbele maendeleo ya kijamii katika dunia inayoendelea.

Utafiti wa mwezi huu uliofanywa na jarida la afya ya jamii nchini Marekani unasema zaidi ya wanawake 1,100 wanabakwa nchini DRC kila siku.

XS
SM
MD
LG