Hisia tofauti zimejitokeza nchini Kenya baada ya Serikali kutangaza kuwa itagharamia kampeni za kupigia debe mapendekezo ya katiba mpya ili wananchi waiunge mkono katika kura ya maoni.
Viongozi wakuu wa Serikali wamesema rasimu ya katiba ni mradi wa Serikali na inajukumu la kuwapa wakenya katiba mpya ambayo wamekuwa wakiisubiri kwa miaka mingi. Duru zinasema viongozi hao wamepanga kufanya kampeni kali licha ya kuwepo pingamizi kutoka kwa viongozi wanaofanya kampeni za kuipinga rasimu ya katiba ambayo wanadai ina kasoro nyingi ambazo zinapaswa kushughulikiwa kwanza.
Kampeni za pande mbili zimeanza kote nchini huku wanasiasa wakijiingiza kwenye malumbano katika majukwaa ya siasa kote nchini humo.
Shughuli hiyo ya rasimu ya katiba inafuatiliwa kwa makini na wakenya wengi na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa . Baadhi ya wanaharakati wanaounga mkono rasimu hiyo ya katiba wamesema serikali haina budi kuhakikisha inatekeleza makubaliano yaliyofikiwa wakati wa kuunda serikali ya pamoja ikiwemo kuwapatia wakenya katiba mpya.
Hata hivyo wanaoipinga wameapa kuendelea na kampeni zao za kuikemea na kuikataa rasimu hiyo kabla ya kufikiwa upigaji kura wa maoni. Na wanasema si haki kwa serikali kutumia fedha za umma kusaidia upande mmoja tu wa mjadala huo.
Hisia tofauti zimejitokeza nchini Kenya baada ya Serikali kutangaza kuwa itagharamia kampeni za kupigia debe mapendekezo ya katiba mpya ili wananchi waiunge mkono katika kura ya maoni.