Chebukati alitangaza uteuzi huo kupitia gazeti rasmi la serikali. Hatua hiyo inampa uwezo naibu wake kutekeleza majukumu yote ambayo mwenyekiti huyo anatunukiwa kikatiba.
Haya yalijiri siku moja baada ya mwenyekiti huyo kukutana na rais Uhuru Kenyatta kwenye afisi ya rais iliyo katika jumba la Harambee House mjini Nairobi.
Wakati huo huo, Jumanne jioni, gari la naibu jaji mkuu nchini Kenya Philomena Mwilu lilishambuliwa kwa risasi kwenye barabara ya Ngong Rd karibu na eneo la duka la jumla la Nakummat.
Dereva wa gari hilo alipata majereha ya risasi mgongoni na akakimbizwa kwa hospitali moja mjini Nairobi.
Jaji mwilu hakuwa kwenye gari hilo.
Kaimu waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang'i alifika kwenye eneo la tukio hilo na kusema kuwa polisi walikuwa wameanza uchunguzi kuhusiana na shambulizi hilo.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alisema kuwa dereva huyo alishambuliwa na watu waliokuwa kwenye pikikipiki alipokuwa akinunua shada la maua.
Mapema Jumanne, raia watatu waliwasilisha kesi kwenye mahakama ya upeo kutaka uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika siku ya Alhamisi kusitishwa.Wakiwakilishwa na mawakili Harun Ndubi, John Khaminwa na Paul Nyamodi, wapiga kura hao wanaotoka kwenye maeneo wakilishi ya Nyali, Westlands na Mathare wameeleza kwamba uchaguzi huo hauwezi kuwa huru na wa haki kwa sababu tume ya IEBC imegawanyika kimsimamo, kati ya masuala mengine.
Jaji mkuu David Maraga alitoa amri kwamba kesi hiyo isikilizwe siku ya Jumatano.
Kesi nyingine iliyowasilishwa na aliyekuwa mbunge wa Kilome, Aron Mwau, ikimtaka rais Kenyatta na naibu wake William Ruto kuondolewa kwa kinyang'anyiro cha urais pia itasikilizwa siku ya Ijumaa.
Kesi nyingine iliyomtaka kinara wa muungano wa upinzani, NASA, kulazimishwa kushiriki kwenye uchaguzi wa Alhamisi, ilitupiliwa mabali na mahakama kuu.
Serikali ya Kenya ilitangaza Jumatano tarehe 25 kuwa sikukuu ya kitaifa.
Haya yalijiri katika siku ambayo maandamano ya kupinga uchaguzi wa Alhamisi yalifanyika katika miji kadhaa, ikiwemo Kisumu na Nairobi.