Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 05:11

Chama cha UDP chadai maandamano ni uchochezi, uvunjifu wa amani


John Cheyo
John Cheyo

Mwenyekiti wa chama cha upinzani UDP nchini Tanzania John Cheyo amesema Jumapili maandamano yaliyopangwa kufanyika April 26, 2018 ni uchochezi na uvunjifu wa amani na kwamba, mambo yanayolalamikiwa yangeweza kutatuliwa kupitia mabaraza ya vyama vya siasa.

Maandamano hayo kwa mujibu wa Cheyo yanaratibiwa kupitia mitandao ya jamiii, gazeti la Mwananchi limeripoti.

Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alivionya vyama vya siasa na wananchi ambao wamepanga kufanya maandamano.

Rais aliwataka waliojiandaa kutekeleza mpango waache mara mora vinginevyo watashughulikiwa.

“Nchi hii ni ya amani, ndiyo maana uvunjifu wa amani ulipoanza kutokea kule Kibiti tuliamua kuufuta mara moja. Kuna watu wanadhani tunafanya siasa kila wakati, kama wametumwa na baba zao kuandamana, watawasimulia vizuri.

Kwa mujibu wa maelezo ya Cheyo mabaraza ya vyama vya siasa yakitumika kikamilifu yanaweza kuondoa malalamiko ya wananchi na viongozi wa upinzani.

"Tusitake kufika hatua ya kuandamana barabarani ili kudai haki, Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi. Tukifikia huko amani iliyopo Tanzania tutashindwa kuipata tena na wananchi watakosa nchi nyingine yenye amani ya kukimbilia," amesema.

Gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa Cheyo alisema kama tatizo ni fedha kwa ajili ya mabaraza hayo kukutana, Rais John Magufuli anapaswa kutoa fedha kuyawezesha kufanya vikao.

"Siungi mkono hoja za kudai kuwepo mikutano ya hadhara hata kama ni kwa ajili ya kuongeza wanachama kama wanavyodai wengine, naamini kwa sasa mitando ya kijamii ina nguvu kuliko kitu chochote nchini," amesema Cheyo.

Amesema kabla ya kudai haki ya kuandamana, zipo nyingine wananchi wapaswa kuzipa kipaumbele zikiwemo haki ya kuishi, kupata maji safi na salama, elimu na afya.

"Hatuwezi kufika mahali tuseme nchi hii imepotea na hakuna demokrasia kisa tumekosa haki ya kuandamana, haki ya kufanya mikutano ya hadhara. Kila mtu alishuhudia mikutano ya kampeni za uchaguzi wa ubunge wa marudio katika majimbo ya Kinondoni na Siha ilivyogeuka sehemu ya kutukanana," amesema Cheyo.

"Kama kitu mnachokidai kiliweza kusababisha watu kugombana na askari hadi mauaji yakatokea hicho kitu hakitusaidii kama nchi," amesema.

Cheyo ameongeza yanayodaiwa kwa nguvu hayana faida na manufaa ya kila siku kwa sababu watu wanahitaji kupata wakati wa kulima na kuvuna.

"Hiyo mikutano iliyoshupaliwa sasa na kuhitajika kwa nguvu zote si kweli kwamba kila siku watakuwa barabarani kuhutubia wananchi, fedha tutatafuta saa ngapi, tutalima saa ngapi, hivyo ni vyema tutambue kila kitu kinachofanyika kupitia mambo ya siasa kisiwe kisingizio cha kusema nchi haina amani, haina uhuru," amesema Cheyo.

Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwa kiunganishi cha wananchi na viongozi wa vyama vya siasa na si kufanya kinyume cha hilo.

XS
SM
MD
LG