Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Februari 08, 2023 Local time: 09:45

Malawi katangaza hatua kali dhidi ya wanyanyasaji kijinsia.


Rais wa Malawi President Lazarus Chakwera mjini Lilongwe, Malawi, Juni 28,2020.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ametangaza mipango ya adhabu kali dhidi ya wale wanaofanya unyanyasaji wa kijinsia, baada ya kuongezeka kwa kesi na aina hiyo wakati wa janga la corona. Katika hotuba yake ya kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Desemba 10, Chakwera alisema Malawi pia itahitaji kufundishwa kwa haki za binadamu mashuleni.

Rais Chakwera alisema takwimu inayoonyeshwa na idara ya taifa ya takwimu za ghasia za kijinsia inaogopesha.

“Miaka mitatu iliyopita, Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu iliripoti kwamba mmoja kati ya wanawake na wasichana watatu wa Malawi kati ya miaka 15 hadi 49 anapata unyanyasaji wa kingono au kimwili. Na kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, kesi za uhalifu huu zimekuwa zikiongezeka. Na katika miezi mitatu iliyopita ya mwaka huu pekee, kiwango kimekuwa juu kwa asilimia 35 kuliko kipindi hicho hicho mwaka jana.” Aliongeza Chakwera.

Chakwera alisema mwelekeo huo unaonyesha kuwa chini ya vizuizi vya kutoka vilivyowekwa ili kupambana na COVID-19, uhalifu wa kijinsia umeenea. Alitangaza mipango ya adhabu kali dhidi ya wale wanaofanya vurugu za kijinsia.

“Wizara za Sheria, Jinsia na utawala zitaandaa marekebisho ya sheria husika ikiwa ni pamoja na Utaratibu wa Makosa ya Jinai na nambari ya Ushahidi ili kuharakisha kushughulikiwa kwa kesi kama hizo, kutoa adhabu kali za lazima dhidi ya wakosaji na kuanzisha sajili ya wahalifu wa kijinsia.”alisema Chakwera.

Chakwera pia alisema Malawi itahitaji kufundishwa kwa haki za binadamu Mashuleni.

Kwa miezi miwili iliyopita, wapigania haki wamekuwa wakifanya maandamano kadhaa dhidi ya kesi zinazoendelea za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia kwa wasichana na wanawake.

Wakati wa maandamano hayo mwezi Novemba, Chama cha Madaktari Wanawake nchini Malawi na wanaharakati wengine wa haki walimpa Rais Chakwera siku 90 kuwasilisha hatua za kusaidia kumaliza unyanyasaji wa kijinsia.

Kesi mpya za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana huripotiwa nchini Malawi karibu kila wiki. Siku ya Alhamisi vyombo vya habari vya viliripoti kuwa polisi katika wilaya ya kusini ya Mangochi wamemkamata mwanamume mwenye umri wa miaka 33 kwa kubaka dada watatu wenye umri kati ya miaka 12 na 14. Mmoja wao sasa ni mjamzito.

Sheria za sasa hazitekelezwi-Kathewera-Banda

Maggie Kathewera-Banda ni mkurugenzi mtendaji wa Harakati za Ilani ya Wanawake.

Anasema shida kubwa ni kwamba sheria za sasa hazitekelezwi.

“Nadhani hatushughulikii maswala halisi, kwa sababu ukiangalia ubakaji ni ipi hukumu ya juu? Wanasema unaweza hata kwenda kwenye hukumu ya kifo. Kwa sababu kwangu, nadhani Malawi ni juu ya utekelezaji wa sheria zetu badala ya sheria zenyewe. Kwa miaka mingi tulijaribu kuja na sheria za jinsia lakini unakuta hazijatekelezwa. ” Alisema Banda.

Immaculate Maluza ni rais wa Chama cha Wanasheria Wanawake nchini Malawi. Anasema mitazamo kuhusu unyanyasaji wa kijinsia lazima ibadilike.

Maluza anasema hatua zinapaswa kuchukuliwa kuharamisha vitendo vya kitamaduni vinavyodhuru unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Imetayarishwa na Sunday Shomari, VOA , Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG