Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Oktoba 08, 2024 Local time: 00:45

Chadema kinaomba viongozi wake waachiliwe mara moja


Freeman Mbowe kiongozi wa CHADEMA akizungumza na waandishi habari
Freeman Mbowe kiongozi wa CHADEMA akizungumza na waandishi habari

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Jumatatu kimeomba kuachiliwa kwa viongozi wake wakuu ambao walishikiliwa katika kamata kamata ya watu wengi kabla ya mkutano wa hadhara wa siku ya vijana uliopigwa marufuku.

Waliokamatwa ni pamoja na mwenyekiti wa chadema Freeman Mbowe na naibu wake Tundu Lissu, wote wakiwa wagombea wa zamani wa urais. Makada wengine kadhaa wa chama walikamatwa pia, kulingana na maafisa wa chama hicho.

Ni miongoni mwa wanachama 469, wakiwemo viongozi na vijana wanachama, waliokamatwa kote nchini, Chadema kimesema katika taarifa, kikiomba waachiliwe mara moja na bila masharti.

Makundi ya haki za binadamu na wapinzani wameelezea wasiwasi wao kuwa hatua hiyo ya polisi inaweza kuashiria kurejea kwa sera za ukandamizaji za hayati rais John Pombe Magufuli wakati nchi inajiandaa kwa uchaguzi wa mwaka ujao.

Kukamatwa kwa wanachama hao wa Chadema kumejiri licha ya mrithi wa Magufuli Rais Samia Suluhu Hassan kuahidi kurejea kwa “ushindani kwenye uwanja wa siasa” na kulegeza baadhi ya vikwazo kwa upinzani na vyombo vya habari, ikiwemo kuondolewa mwezi Januari mwaka 2023 kwa marufuku ya miaka sita ya mikutano ya vyama vya upinzani.

Maafisa wa Chadema wamesema Mbowe, alikamatwa Jumatatu kwenye uwanja wa ndege wa mji wa kusini magharibi wa Mbeya, siku moja baada ya viongozi wengine kadhaa akiwemo Lissu kushikiliwa.

Forum

XS
SM
MD
LG