Idadi ya vifo kutokana na moto ulioteketeza ghala moja mjini Oakland California imefikia 33 Jumapili na huenda ikaongozeka hadi 40 wakati waokozi wakiendelea kutafuta kwenye mabaki ya jengo hilo ambapo densi iliorembeshwa kieletroniki ilishika moto.
Kufikia Jumapili usiku , ni asilimia 20 pekee ya jengo hilo iliokuwa imefikiwa. Afisa Melinda Dayton kutoka idara ya zima moto alisema kuwa shughuli ya uokozi haikuwa rahisi lakini akaongeza kuwa heshima ya waathirika pamoja na familia zao ingedumishwa.
Moto ulizuka Ijumaa kwenye jengo hilo lililozeeka na ambalo liligeuzwa kuwa studio ya muziki. Inasemekana kuwa hakukuwa na kibali cha jengo hilo kutumika kama makazi ya binadamu au hata eneo la burudani. Maafisa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kiini cha moto huo.