Maafisa wa kijasusi wa Burundi waliwakamata wanaharakati watano, wanne kati yao walikuwa wakitarajiwa kupanda ndege mwezi uliopita kutoka mji mkuu wa kibiashara wa Bujumbura kuelekea Uganda.
Baadaye walishtakiwa kwa uasi na kuhatarisha usalama wa ndani ya nchi pamoja na kudumaza utendaji wa masuala ya fedha za umma, kabla kukamatwa na kuzuiliwa kwenye gereza kuu mjini Bujumbura.
Kulingana na kifungu cha sheria za Burundi, watuhumiwa wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 30 jela.
Mashirika yanayotetea haki za binadamu ya Amnesty International, Human Rights Watch (HRW) na Shirika la Haki za Kibinadamu la Burundi yalisema mashtaka dhidi ya wanaharakati hao "hayana msingi" na kutaka yafutwe
"Ukamataji huo ... na kufunguliwa mashtaka makubwa dhidi yao kunaashiria hali mbaya zaidi kwa jamii huru za kiraia nchini Burundi," alisema Clementine de Montjoye, mtafiti wa Afrika katika shirika la Human Rights Watch.
Wanaharakati walioko jela ni pamoja na rais wa Chama cha Wanasheria Wanawake Burundi Sonia Ndikumasabo, ambaye alikamatwa akiwa uwanja wa ndege.
Mtu mwingine ni Prosper Runyange, mwanachama wa Chama cha Amani na Kukuza Haki za Binadamu (APDH), aliyekamatwa siku hiyo hiyo katika mji wa Ngozi ulioko wa kaskazini mwa nchi hiyo.
"Kama kufanya kazi kwa kushirikiana au kupokea ufadhili kutoka kwa makundi ya kimataifa kutachukuliwa kama kosa la jinai na tishio kwa usalama wa taifa, nafasi ndogo iliyoachwa kwa mashirika ya kiraia kufanya kazi zake nchini Burundi itafungwa kabisa” Montjoye wa Human Rights Watch alionya.
Licha ya wasiwasi unaoendelea kuhusu haki za binaadamu, Umoja wa Ulaya na Marekani mwaka jana zilianza tena kutoa mtiririko wa misaada kwa taifa hilo maskini lisilo na bandari, kwa kuelezea maendeleo ya kisiasa yaliyofanywa chini ya Rais Evariste Ndayishimiye.
Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP.
Facebook Forum