Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Oktoba 12, 2024 Local time: 22:01

Burundi: Waziri mkuu wa zamani akamatwa


Waziri mkuu wa zamani wa Burundi Alain Guillaume Bunyoni.
Waziri mkuu wa zamani wa Burundi Alain Guillaume Bunyoni.

Waziri mkuu wa zamani wa Burundi Alain Guillaume Bunyoni alikamatwa na anaendelea kuhojiwa na polisi, mwendesha mashtaka mkuu alisema Jumapili.

Katika taarifa yake, mwendesha mashtaka Sylvestre Nyandwi alisema Jenerali Bunyoni alikamatwa siku ya Ijumaa katika mtaa wa Mubone wilaya ya Kabezi, kusini mwa mji mkuu Bujumbura, ambako alikuwa amejificha. Nyandwi aliongeza kuwa “ Nilitoa hati ya kuendesha msako nyumbani kwa Bunyoni tarehe 17 Aprili, lakini polisi hawakumkuta nyumbani kwake.”

‘Baadaye nlitoa hati ya kumkamata,” Nyandwi alisema.

Nyandwi alisema polisi wanaendelea kukusanya ushahidi wa makosa ya uhalifu “ambayo Bunyoni anaweza kuwa alifanya, na ushahidi huo utawasilishwa kwa mwendesha mashtaka mkuu, naye achukuwe hatua za kisheria baadaye.”

Bunyoni, kigogo mwenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha CNDD-FDD ambaye aliteuliwa kama waziri mkuu mwaka wa 2020, alifutwa kazi siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuonya kuhusu “jaribio” la mapinduzi dhidi yake.

Ndayishimiye alichukua madaraka mwezi Juni mwaka wa 2020 baada ya mtangulizi wake Pierre Nkurunziza kufariki kutokana na kile maafisa walisema ni mshtuko wa moyo licha ya uvumi uliosambaa kwamba alifariki kutokana na Covid 19.

Jenerali Bunyoni ambaye aliwahi kuwa waziri wa usalama na mkuu wa polisi, yuko chini ya vikwazo vya Marekani kwa tuhuma za kuhusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa maandamano ya mwaka wa 2015 ya kupinga muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza.

XS
SM
MD
LG