Kura zinahesabiwa nchini Burundi ambako ghasia za kabla ya uchaguzi zilisababisha maelfu ya watu kuondoka nchini humo katika miezi ya hivi karibuni.
Uchaguzi huo wa rais wenye utata ulifanyika jumanne na unaaminiwa kuwa watu kidogo walijitokeza kupiga kura, pale rais Pierre Nkuruzinza alipowania muhula wa tatu bila ya kuwa na mpinzani mkubwa.
Matokeo rasmi ya uchaguzi yanatarajiwa kutolewa alhamisi. Lakini uchaguzi huo umekosolewa kwa kutokuwa huru na wa haki, baada ya serikali kupuuza mgomo wa upande wa upinzani na wito kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kuaakhirisha uchaguzi kwa ajili ya hali ya ghasi ilojiri.
Maafisa wa serikali wanaripoti kuwa takriban watu watatu waliuwawa, polisi wawili na afisa mmoja wa upinzani, katika mashambulizi ya jumatatu usiku kabla ya uchaguzi.
Idhaa ya afrika ya kati ya Kirundi/ Kinyarwanda ya sauti ya amerika, iliripoti kwamba mji mkuu Bujumbura ulikuwa shwari wakati wa upigaji kura. Mashahidi wanasema vituo vya kupiga kura vilikuwa na harakati nyingi katika kijiji cha Buye anakotokea rais, na sehemu nyenginezo za nchi zenye zinazomuunga mkono Nkuruzinza.
Wakosoaji wanasema Bw. Nkuruzinza hapaswi kuwania muhula wa tatu, lakini Mahakam ya kikatiba ya Burundi iliamuwa kuwa anaweza kufanya hivyo kwa sababu alichaguliwa na wabunge na sio wapiga kura katika muhula wake wa kwanza kama rais hapo mwaka 2005.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema jumanne kwamba kwa kuendelea na uchaguzi, serikali ya Burundi inaweza kupoteza uhalali wake kwenye macho ya watu wake na kuharibu makubaliano ya Arusha ambayo yalipelekea kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani inasema kuwa takriban raia wa burundi elfu mia moja na sitini na saba wametoroka nchi hiyo kukimbia ghasia.
Uchaguzi wa rais unafwatia uchaguzi wa bunge ulofanyika mwezi ulopita, ambao chama cha rais Nkuruzinza kilishinda kwa urahisi. Upinzani pia uligomea uchaguzi huo, ambao ulikashifiwa kimataifa kwa kutokuwa wa huru na wa haki.
Wagombea wa upinzani wameelezea hisia hizo hizo kwa uchaguzi wa rais, wakisema vitisho viloenea na kitisho cha ghasia kunazuia nchi hiyo kuweza kufanya uchaguzi ulokuwa wa huru na wahaki.