Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 12:43

Marekani inaunga mkono jitihada za Tanzania-Perriello


 Mwakilishi maalum wa Marekani katika nchi za maziwa makuu Tom Perriello
Mwakilishi maalum wa Marekani katika nchi za maziwa makuu Tom Perriello

Mwakilishi maalum wa Marekani katika nchi za maziwa makuu anayeshughulikia mgogoro wa Burundi Thomas Periello amesema Marekani inaunga mkono jitihada zinazofanywa na mpatanishi wa mgogoro huo Rais mstaafu wa Tanzania Benjamini Mkapa lakini akibainisha kwamba hali ya usalama ya Burundi bado si shwari.

Bwana Perrielo alikuwa akizungumza na Sauti ya Amerika katika mahojiano maalum kwenye ubalozi wa Marekani jijini Dar es salaam kuhusu mazungumzo ya amani ya mgogoro wa Burundi yanayofanyika jijini Arusha baina ya pande zinazohasimiana nchini humo ambapo yeye amehudhuria.

Amesema vyama vya siasa nchini Burundi vimekuwa ni kikwazo katika kufikia amani nchini humo na kuendelea kusababisha hali tete ya usalama ikiwamo mauaji ya watu wasio na hatia akitolea mfano kuuawa hivi karibuni kwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Hafsa Mossi.

Akizungumzia suluhisho la mgogoro wa burundi na maeneo mengine yenye migogoro katika ukanda huo Bwana Perriello amesema ni kwa serikali za nchi hizo kuzingatia ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya kidemokrasia ili kuleta amani ya kudumu katika nchi zao.

Katika hatua nyingine mjumbe huyo maalum wa Marekani katika nchi za maziwa makuu ambaye amepata pia kushughulikia migogoro huko Siera Leone na Darfur, ameeleza kuridhishwa na juhudi za Tanzania katika kusuluhisha migogoro mbalimbali ikiwemo pia kuhifadhi wakimbizi wanaotokana na migogoro hiyo katika nchi za maziwa makuu.

XS
SM
MD
LG