Imekuwa rasmi: Chama tawala nchini Burundi cha CNDD-FDD kimemteuwa Rais wa sasa wa Burundi Pierre Nkurunziza kukiwakilisha katika uchaguzi wa urais wa mwezi Juni mwaka huu.
Hatua hiyo imechukuliwa katika kongamano kuu la chama lililofanyika Jumamosi Aprili 25 jijini Bujumbura na kuhudhuriwa na wafuasi 898 kwa jumla ya 1020 waliyokuwa wamealikwa. Hatua nyingine iliyochukuliwa katika kongamano hilo ni kuwavuwa uwanachama wafuasi zaidi ya 30 waliopinga rais kugombania muhula wa tatu katika uchaguzi wa mwaka huu.
Imekuwa pia fursa ya kumsimamisha katika baraza la wazee wa busara wa chama hicho Bwana Gervais Rufyikiri ambaye ni makamu wa pili wa rais na Pie Ntavyohanyuma spika wa baraza la bunge baada ya maafisa hao kudhihirisha msimamo wao wa kupinga uwezekano wa rais Nkurunzinza anayeongoza Burundi tangu mwaka wa 2005 kugombea urais kwa mara ya tatu mwaka huu.
Hatua hiyo imepokelewa kwa huzuni na upinzani pamoja na baadhi ya mashirika ya kiraia nchini Burundi. Kwa mujibu wa makundi hayo ni ukiukwaji mkubwa wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa ili kusitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi na katiba ya Burundi.
Jamii ya kimataifa, ikiwa na pamoja na Umoja wa Ulaya, kanisa katoliki lenye wafuasi wengi nchini humo, Marekani na Umoja wa Mataifa walionyesha upinzani wao dhidi ya muhula wa tatu wa rais wa sasa wa Burundi Pierre Nkurunziza kwa njia mbali mbali.
Pengine athari ya hatua hiyo itaonekana kuanzia kesho Jumapili alfajiri iwapo wananchi wanaopinga Rais Nkurunziza kugombea muhula wa tatu watiatikia wito wa mashirika ya kiraia na vyama vya upinzani na hivyo kuteremka barabarani kufanya mandamano ya amani kwa ajili ya kuonyesha upinzani wao dhidi ya hatua hiyo ya chama tawala.
Kwa hivi sasa hofu imetanda miongoni mwa wananchi katika taifa lote.Takriban zaidi ya wananchi elfu nane walitoroka nchi wakihofia ghasia za uchaguzi ambazo zinaweza kuchochewa na utofauti uliopo kutokana na swala hilo la muhula mwengine wa Rais Nkurunziza.