Wafanyakazi wa uchaguzi huko Burundi wanaendelea na zoezi la kuhesabu kura kufuatia uchaguzi wa serikali za mitaa, ikiwa ni wa kwanza katika mlolongo wa upigaji kura na mtihani kwa uthabiti wa taifa hilo la afrika yakati.
Upigaji kura jana Jumatatu uliongezwa kwa saa mbili katika baadhi ya wilaya huku mistari mirefu ikiripotiwa kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Raia wa Burundi wapatao milioni 3.5 walistahili kupiga kura kwenye uchaguzi wa kwanza katika mlolongo wa chaguzi hadi September ambapo hatimaye watachagua rais na bunge.
Maafisa waliahirisha upigaji kura mara mbili tangu Ijumaa wakisema walihitaji muda zaidi kugawa karatasi za kupigia kura katika baadhi ya maeneo na kwamba baadhi ya watu hawakuwa na kadi za kupigia kura.