Kesi inayowakabili watuhumiwa 28 wa jaribio la kupindua Serikali ya Burundi yaliofeli Mei Mwaka wa 2015, imepangwa kuanza kusikilizwa Jumatatu tarehe Saba Machi, 2016 kutokana na ombi la mwendesha mashitaka.
Jaribio hilo ni moja wapo ya matukio na migogoro ya kisiasa ambayo yameendelea kushuhudiwa nchini Burundi tangu Aprili mwaka jana pale Rais Pierre Nkurunziza alipotangazwa na chama chake kuwa mgombea urais kwa muhula wa tatu.
Kesi ya watuhumiwa hao imepangwa kusikilizwa katika mahakama ya mkoa wa kati kati mwa Burundi wa Gitega ambako wote wanazuiliwa miongoni mwao wakiwa ni Askari Jeshi na Polisi wa kawaida.