Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Machi 26, 2025 Local time: 20:53

Uingereza yawafukuza wanadiplomasia wa Libya


Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague akizungumza na vyombo vya habari huko London, kwamba Uingereza inalitambua rasmi baraza la kitaifa la mpito nchini Libya
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague akizungumza na vyombo vya habari huko London, kwamba Uingereza inalitambua rasmi baraza la kitaifa la mpito nchini Libya

Uingereza imewafukuza rasmi wanadiplomasia wote wa utawala wa kiongozi wa Libya Moammar Gadhafi na kulitambua Baraza la Kitaifa la Mpito linaloongozwa na upinzani kama serikali halali nchini humo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague alisema Jumatano hatua hiyo ililenga kuinua uhalali wa upinzani, uwezo na mafanikio ya kuwafikia wa-Libya nchini kote. Alisema Uingereza itafanya kazi na Baraza hilo kama inavyofanya kazi na serikali zote kote duniani.

Hague alisema Baraza la Kitaifa la Mpito linafanya kazi kuelekea uwazi zaidi na demokrasia nchini Libya kinyume na utawala wa bwana Gadhafi ambapo ghasia dhidi ya watu wa Libya zimempotezea uhalali wake wa kuwepo madarakani.

Marekani, Ufaransa na zaidi ya nchi 30 nyingine zinalitambua Baraza hilo la Mpito kama serikali ya muda nchini Libya.

Hague alisema juhudi za jeshi la jumuiya ya kimataifa zimeokoa maisha ya maelfu ya watu nchini Libya. NATO imefanya mashambulizi ya anga chini ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuwalinda raia.

Hague pia alitangaza Uingereza imeachia dola milioni 149 ilizodhibiti kutoka kwa serikali ya Libya ili kuwasaidia watu wa Libya. Uamuzi wa Uingereza kuutambua upinzani umetangazwa siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Libya kusema suala la kuondoka kwa bwana Ghadhafi halipo kwenye mazungumzo.

Al-Baghdadi al-Mahmoudi pia alisema Jumanne hakutakuwa na njia yoyote ya mazungumzo juu ya mgogoro wa kisiasa wa Libya hadi kwa maneno yake “NATO isitishe hatua zake za kimabavu.”

Alitoa matamshi hayo baada ya mazungumzo na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa Abdul Elah al-Khatib ambaye alikutana na upinzani nchini Libya siku ya Jumatatu mjini Benghazi.

XS
SM
MD
LG