Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 14:58

Mlipuko wa bomu wauwa nchini Nigeria


Wafanyakazi wa idara ya dharura Nigeria wakifanya kazi katika eneo la tukio ambapo mtu mmoja alikufa na magari kadhaa yaliharibiwa huko Abuja. June 16,2011.
Wafanyakazi wa idara ya dharura Nigeria wakifanya kazi katika eneo la tukio ambapo mtu mmoja alikufa na magari kadhaa yaliharibiwa huko Abuja. June 16,2011.

Bomu moja lenye nguvu limelipuka nje ya makao makuu ya polisi nchini Nigeria, katika mji mkuu wa Abuja na kumuuwa mtu mmoja.

Maafisa wa idara ya dharura nchini Nigeria wanasema wanashuku mlipuaji wa kujitoa mhanga ndie aliyefanya shambulizi hilo na alikufa katika mlipuko.
Katika mahojiano na Sauti ya Amerika-VOA, msemaji wa kundi la wanamgambo wa ki-Islam la Boko Haram alidai kuhusika kwa bomu hilo.

Kundi la Boko Haram limekuwa likilaumiwa kwa kufanya mifululizo ya mashambulizi kaskazini-mashariki mwa Nigeria ambayo ililenga maafisa wa polisi, serikali na viongozi wengine wa serikali.

Mlipuko wa bomu wa Alhamisi ulitokea katika eneo la kuegeshea magari karibu na makao makuu ya polisi. Televisheni ya Nigeria ilionyesha picha za video zinazoonyesha moshi mzito mweusi ukizagaa kutoka kwenye magari yaliyoharibika.

Maafisa wa zimamoto na waokozi wapo katika eneo la tukio na polisi wamefunga barabara zote zinazoelekea katika eneo la tukio.
Shirika la habari la Reuters linamkariri msemaji wa chama cha msalaba mwekundu akisema shirika hilo linabeba miili na kuwahudumia majeruhi katika eneo lililoshambuliwa.

Nigeria imekuwa ikishambuliwa kwa mabomu mara kwa mara kutokana na mivutano ya kisiasa.

Mwezi Oktoba mwaka jana, watu 12 walikufa katika mabomu mfululizo ndani ya gari mjini Abuja katika siku ya uhuru wa Nigeria. Maafisa walililaumu shambulizi hilo kwa wanamgambo kutoka eneo tete nchini humo la Niger Delta.
Kundi la Boko Haram linaaminika kufanya mashambulizi mengi huko kaskazini-mashariki mwa Nigeria, hasa katika jimbo la Borno. Kundi hilo linashinikiza kuwepo na sheria kali ya ki-Islam huko kaskazini.

XS
SM
MD
LG