Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amekutana mjini Amman leo Jumanne na viongozi wa juu wa Jordan na mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa Gaza, huku kukiwa na msukumo wa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas na kufikisha misaada zaidi katika Ukanda wa Gaza.
Blinken alifanya mazungumzo tofauti pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi na Mfalme Abdullah II, kabla ya mkutano wake na Sigrid Kaag, mratibu mwandamizi kwenye Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu na ujenzi mpya kwa Gaza.
Wakati wa mkutano wake na Abdullah, Blinken alijadili juhudi za kufikia makubaliano ya sitisho la mapigano ambalo litapelekea kuachiliwa kwa mateka na kusisitiza kuwa Hamas inapaswa kukubali pendekezo lililopo mezani.
Blinken pia alijadili juhudi za kidiplomasia zinazoendelea ili kufikia amani ya kudumu katika eneo hilo, ikijumuisha kufungua njia kuelekea taifa huru la Palestina na dhamana ya usalama kwa waisraeli.
Forum