Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 05:05

Biden kukutana na viongozi wa Australia, India na Japan


Bendera za nchi za "Quad"
Bendera za nchi za "Quad"

Rais wa Marekani Joe Biden atakuwa mwenyeji wa mkutano wa kwanza ana kwa ana na viongozi wenzake wa nchi ziitwazo "Quad" - Australia, India, Japan na Marekani - ambazo zimeonyesha azma ya  kuongeza ushirikiano kukabiliana na uthubutu na ushawishi unaoongezeka wa China.

Mkutano huo utafanyika katika Ikulu mjini Washington DC tarehe 24 mwezi huu wa Septemba, msemaji wa White House Jen Psaki alisema katika taarifa.

Ziara hapa Marekani za mawaziri wakuu wa Australia, India na Japan - Scott Morrison, Narendra Modi na Yoshihide Suga - zitaenda sambamba na mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, ambao Biden atahutubia tarehe 21 mwezi huu.

Katika mkutano kwa njia ya mtandao wa viongozi wa Quad mnamo mwezi Machi mwaka huu, waliahidi kushirikiana kwa karibu katika masuala ya chanjo za COVID-19, na hali ya hewa na kuhakikisha eneo la Indo-Pacific liko huru na wazi licha ya changamoto kutoka Beijing.

"Kukaribisha viongozi wa Quad kunaonyesha kipaumbele cha utawala wa Biden-Harris cha kushirikiana na nchi za Indo-Pacific, pamoja na kuweka mikakati mipya ya pande zote ili kukabiliana na changamoto za karne ya 21," Psaki alisema.

Biden, ambaye anasukuma mpango wa matumizi makubwa fedha kwa miundombinu nchini mwake, alisema mwezi Machi mwaka huu kwamba alikuwa amependekeza kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kuwa nchi za kidemokrasia zinapaswa kuwa na mpango wa miundombinu ya kupingana na mpango mkubwa wa China uitwao Belt and Road, ambao una miradi kutoka Asia Mashariki hadi Ulaya, na hata barani Afrika.

Mjini Beijing siku ya Jumanne, msemaji wa wizara ya mambo ya nje alisema, "China inaamini mfumo wowote wa ushirikiano wa kikanda unapaswa kwenda na mwenendo wa nyakati na uwe mzuri."

Msemaji, Zhao Lijian, alisema mikutano "haipaswi kulenga mtu yeyote wa tatu."

XS
SM
MD
LG