Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Machi 04, 2024 Local time: 02:18

Tanzania yaahidi kuendelea kupambana na biashara ya ngono na ushoga


Dkt Kigwangalla
Dkt Kigwangalla

Serikali ya Tanzania imeonya kuwa adhabu kali itatolewa kwa mtu atakayebainika kufanya vitendo vya jinsi moja ambayo ni kifungo cha zaidi ya miaka 30 jela.

Pia imeahidi kuendelea kupambana kwa nguvu zote na vitendo vya mapenzi ya jinsi moja na kwamba, mwanamume atakayethibitika kufanya vitendo vya kike (ushoga) ataadhibiwa kisheria.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Hamisi Kigwangalla ameeleza hayo Ijumaa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo.

Mbunge huyo amesema kumekuwa na biashara kati ya wanaume na wanawake lakini pia ipo ya watu wa jinsi moja. “Nataka kufahamu hao wanachukuliwa hatua gani?” amehoji Lyimo.

Naibu waziri amesema sheria inakataza watu wa jinsi moja kufanya mapenzi kinyume cha maumbile na pia inakataza wanaume kufanya vitendo vya jinsi ya kike.

Amesema kuwa Serikali imekuwa ikipambana kwa nguvu zote na makundi haya ambayo yamekuwa yakishiriki katika vitendo vya mapenzi ya jinsi moja, wakihamasisha ama kuhalalisha au kufanya yaonekane kama kitu cha kawaida .

Dkt Kigwangalla amesema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya operesheni nchi nzima. Amesema taasisi mbalimbali ambazo zilikuwa na mwelekeo wa kutekeleza afua za kinga katika sekta ya afya wamezifuta na kuzibadilisha.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Costantine Kanyasu amehoji kazi ya kuwakamata wanawake wanaojiuza imefanikiwa kwa kiasi gani nchini.

Dkt Kigwangalla amesema tatizo hilo ni kubwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.

“Kitendo cha mwanamke kuishi akitegemea kipato chake au sehemu ya kipato chake kutokana na ukahaba ni kosa la kisheria,” amesema.

Naibu waziri amesema katika kutekeleza sheria ipasavyo, viongozi katika mikoa ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa wakikamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ya wanawake wanaojiuza.

Amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wataendelea kuhakikisha wanawake wanaojihusisha na biashara hiyo wanaendelea kukamatwa ili kulinda heshima, utu na hadhi ya wanawake wa Tanzania.

XS
SM
MD
LG