Polisi wameendelea kuizunguka nyumba ya rais wa chama cha upinzani cha FDC Kiiza Besiigye. Polisi wamemzuia Besigye asiondoke nyumbani mwake wakisema kila wakati Besigye anapotoka nyumbani ufuatwa na watu wanaozua ghasia na kwa sasa hawawezi kumruhusu kutoka nyumbani mwake kwa sababu wanafunzi wa kidato cha nne wanafanya mitihani ya mwisho.
Besigye alikamatwa kwa muda siku ya jumanne na kurudishwa nyumbani kwake na polisi na kufikia Alhamisi hajaruhusiwa kutoka nje.
Alikamatwa alipojaribu kushiriki kwenye maandamano ya kutembea kwenda kazini kupinga ufisadi Serikalini na pia kupinga ongezeko la bei ya chakula.
Zaidi ya polisi mia moja wameizunguka nyumba ya Besigye ili kuhakikisha kuwa hatoki nje .
Naibu kamanda wa polisi mjini Kampala Sam Omala anasema Besigye akitoka nje ya nyumba yake anapanga kuzua ghasia wakati ambao wanafunzi wa kidato cha nne wanapofanya mtihani. Hata hivyo afande Omala alikanusha madai kuwa Besiggye yuko chini ya kifungo cha nyumbani.
Alisema Daktari Kiiza Besigye yuko chini ya kizuizi cha nyumbani na hii ni kulingana na sheria ambayo inaruhusu kumzuia mtu yeyote anayepanga kuzua ghasia asitekeleze mpango wake.
Kamanda Omala anasema kwa sasa hatapiga hata hatua moja kutoka kwenye nyumba yake lakini hivi karibuni ataachiliwa lakini haimaanishi kwamba ataachiliwa kesho.
Besigye anasema kufikia sasa hajaelezewa na polisi ni kwa nini wamemzingira au ni lini wataondoka nyumbani kwake.
Kando na hayo Besigye analalamika kuwa maafisa wa polisi wameanza kuliaribu shamba lake kwa kulitumia kama choo madai ambayo yanakanushwa na kamanda Omala.