Waziri mkuu aliyekua mashuhuri wa Italia na aliyezusha aina mbali mbali za kashfa mnamo miaka 17 ya utawala wake, Berlusconi, amelazimika kujiuzulu Jumamosi kutokana na mzozo wa kiuchumi na kupoteza ungaji mkono bungeni.
Umati mkubwa wa watu ulikusanyika nje ya ikulu ya rais mjini Rome Jumamosi usiku, wakati msafara wa magari ya Berlusconi ulipofika. Alipokelewa kwa hasira na watu hao walomzomea na kumtukana wakimwita mwizi, walimtaka ajiuzulu, hata hivyo katika maeneo mengine alishangiliwa.
Bw. Berlusconi alikutana na Rais Giogrio Napolitano kwa saa moja na kumkabidhi barua yake ya kujiuzulu. Mara moja habari zilisamba kote Rome na sherehe zikaanaza watu wakicheza barabarani na sauti ya mtu moja kusikika akisema "hatimae tuko huru," maoni yanayo chukuliwa kua ni ya Wataliana wengi.
Kamishna wa zamani wa Umoja wa Ulaya Mario Monti, anatazamiwa kuidhinishwa na rais kuchukua wadhifa wa waziri mkuu. Jukumu lake ni kuleta uthabiti katika uchumi ili kuweza kutayarisha uchaguzi mkuu mapema mwakani.