Rais wa Sudan, Omar al-Bashir ameagiza kufunguliwa mpaka wa nchi yake na Sudan Kusini kwa mara ya kwanza tangu kusini ilipojitenga na kuwa taifa huru mwaka 2011.
Shirika la habari la serikali ya Sudan lilisema Jumatano kwamba rais aliwaagiza maafisa wahusika kufanya hatua zote zinazohitajika kutekeleza uamuzi huu wa kufunguliwa mpaka. Uamuzi wa Jumatano ulikuwa hatua moja kubwa kuelekea kuimarisha uhusiano kati ya mataifa haya jirani ambayo kila mmoja amekuwa akimnyooshea kidole mwenzie tangu Sudan kusini ilipojitenga.
Kusini ilichukua sehemu kubwa ya rasilimali za mafuta za Sudan lakini ilikubali kuilipa Kaskazini ada ya kusafirisha mafuta kupita kwenye mabomba yake.
Rais Bashir amekubali kutafakari juu ya kufuta ada hizo. Pande zote mbili pia bado zinagombana juu suala na mpaka pamoja na udhibiti wa kituo kingine kikubwa cha mafuta.