Wajumbe wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walimaliza mazungumzo yao kwa kusisitiza kwamba ni lazima mkataba wa amani ya Somalia utekelezwe na serikali ya mpito lazima imalize muda wake ili kutoa fursa ya demokrasia na amani kwa nchi hiyo.
Mkutano huo ulofanyika Nairobi na kumalizika Jumatano usiku ulihudhuriwa na pande zote husika, pamoja na wajumbe wa majimbo yaliyojitenga ya Puntland na Galmadoug na wadau wengine, na umekamilika bila ya suluhisho maalum, lakini kuitaka serikali ya mpito kuchukua hatua za kutanzua matatizo yao kwa haraka.
Akizungumza na Sauti ya Amerika, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia Balozi Augustine Mahiga, alisema rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed na spika wa bunge la serikali hiyo ya mpito rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, walihimizwa kupatana na kuwa na sauti moja ili juhudi za kurejesha uthabiti wa taifa hilo ziweze kufanikiwa.
Dr Mustafa Ali anaewakilisha makundi ya kutetea haki za kiraia anasema wajumbe kwenye mkutano wamhimiza mashirika ya misaada ya kimataifa na makundi ya kutetea haki za kiraia kuhama kutoka Nairobi na kufunguwa afisi zao mjini Mogadishu.