Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 08:09

Baraza la mawaziri Sudan Kusini laidhinisha mfumo mpya wa utawala


Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir

Baraza la mawaziri la rais wa Sudan kusini Salva Kiir, Jumatano liliidhinisha uamuzi wa kurejesha nchi hiyo katika mfumo wa utawala wa majimbo 10, pamoja na maeneo matatu ya utawala. 

Hatua hiyo inajiri siku chache kabla ya siku ya mwisho iliyowekwa kwa viongozi wa nchi hiyo kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Msemaji wa serikali ya Sudan kusini Michael Makuei, aliiambia Sauti ya Amerika kwamba baraza la mawaziri lilikubaliana kufanyia marekebisho makubaliano ya amani yaliyoafikiwa Agosti 2018 na kuongeza maamuzi ya kurejesha nchi hiyo katika utawala wa mfumo wa majimbo 10 kutoka majimbo 32 ya sasa.

“Baraza la mawaziri limepitisha swala hilo na kumuelekeza waziri wa haki kufanya haraka na kulijumulisha katika katiba ya serikali ya mpito ili lipitishwe kwa sababu hatuna mda kabisa” amesema Makuei katika mahojiano na kipindi cha ssauti ya Amerika kinachoangazia maswala ya Sudan kusini (south Sudan in focus)

Hatua ya Salva Kiir

Mapema wiki hii, rais Kiir alikubali kupunguza idadi ya majimbo kufuatia shinikizo kali kutoka kwa vyama vya upinzani.

Mfumo wa majimbo 32 ulianzishwa na rais Kiir wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano na nusu ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 380,000 na mamilioni kukimbilia nchi jirani, wengi wao wakiishi Uganda kama wakimbizi kwa kuhofia usalama wao.

Rais Kiir, ameunda maeneo matatu ya utawala, ya Pibor, Ruweng na Abyei, hatua ambayo inapingwa na mpinzani wake Dkt Riek Machar.

Kiir na kiongozi wa upinzani Riek Machar wanakabiliwa na shinikizo la kimataifa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kabla ya jumamosi hii, baada ya kushindwa kufanya hivyo mara mbili.

Makuei amesema huenda rais Kiir akasaini mabadiliko hayo na kuwa sheria siku ya ijumaa.

Upinzani watoa msimamo

Naibu wa msemaji wa chama kikuu cha upinzani SPLM-IO Peter Gatkuth, alisema chama hicho hakipingi siku ya mwisho, Februari 22 2020, iliyowekwa kwa ajili ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa lakini kinataka kuona makubaliano yote ya mkataba wa amani yakiwemo ya kiusalama, yakitekelezwa kwanza.

“Angalau asilimai 90 ya maswala yenye utata kama mfumo wa majimbo 10 yameshughulikiwa. Tunaunga mkono hatua hiyo ya rais na pia tunataka swala la eneo la utawala la Ruweng kujadiliwa” Amesema Gatkuoth katika mahojiano na makala ya VOA ya Sudan Sudan in focus.

Ruweng in mojawapo ya maeneo matatu ya utawala yaliyopendekezwa na rais Salva Kiir. Linapatikana kaskazini mwa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta. Wapiganaji wanaoongozwa na Dkt. Riek Machar walipigana sana na wanajeshi wa serikali kudhibithi Ruweng.

Mda unayoyoma

Msemaji wa serikali Michael Makuei alisema maafisa wanastahili kusonga mbele kwa haraka na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kabla ya siku ya mwisho iliyowekwa, akiongezea kwamba mipangilio yote ya usalama imekamilika.

“Tumetoa mafunzo kwa vikosi vya maafisa wa usalama wa kuwalinda watu maarufu na wanasubiri tu kuanza kazi wakati wowote.. hata kesho. Watafanya kazi hapa Juba kuwalinda watu mashuhuri. La pili, wanajeshi wamepewa mafunzo ya kutosha”, amesema Makuei katika mahojiano na waandishi wa habari mjini Juba.

Makuei amesema swala la kuunda kwa serikali ya umoja wa kitaifa halitashikwa mateka kwa sababu baadhi ya makubalino hayajatekelezwa.

Shinikizo za kimataifa

Marekani ilionya mwaka uliopita kwamba itawekea vikwazo vikali mtu yeyote anayehujumu juhudi za kuleta amani nchini Sudan kusini.

Mkuu wa kanisa katoliki Papa Francis na kiongozi wa kanisa la Anglikana, askofu wa Canterbury Justin Welby, wameahidi kwamba watatembelea Sudan kusini baada ya Kiir na Machar kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

-Imetayarishwa na mwandishi wa VOA Kennes Bwire, Washington DC.

XS
SM
MD
LG